Waathirika wa mafuriko Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamepatiwa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 50 kwa lengo la kuwasaidia walioathirika zaidi na mafuriko hayo ili waweze kujikimu kimaisha wakati Serikali ikiendelea kufanya tathmini ya kina.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka, Disemba 12, 2023, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima amesema wananchi zaidi ya 4700 wameathiriwa na mafuriko hayo huku nyumba 997 zilizingirwa na maji kati ya hizo nyumba 85 zimesombwa na maji kabisa.
"...hiki tulichokusanya ndiyo hicho hicho tunapeleka Kilosa hadi sasa sisi Mkoa... tumekusanya mali zenye thamani ya shilingi milioni 50...” amesema Mhe. Adam Kighoma Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo madaraja manne, Barabara na mashamba vyakula na mali nyingine huku watu wawili wakiripotiwa kufariki kutokana mafuriko hayo.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amerudia maelekezo aliyoyatoa hivi karibuni kwa wananchi wa kilosa kutodharau ushauri wa wataalam wa kutorudi kwenye nyumba zao bila kujiridhisha kwa wataalam hao hususan zilizothiriwa sana na mafuriko huku akibainisha kuwa nyumba hizo haziko salama kwa kuwa zimenyonya maji mengi na muda wowote zinaweza kuanguka na kuleta madhara makubwa.
Sambamba na agizo hilo Mhe. Malima ameishukuru Serikali, wadau mbalimbali wa maendeleo na chama cha mapinduzi kwa kuungana pamoja katika kuwasaidia wananchi wa Kilosa waliokumbwa na kadhia hiyo ya mafuriko.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka ameishukuru Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa, Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na Wilaya pamoja na wadau waliotoa misaada hiyo na kwamba Serikali inawajali wananchi wake.
Aidha, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha shilingi bilioni 13 kwa ajili kuboresha miundombinu ndani ya Wilaya hiyo kwa lengo la kupunguza maafa huku akibainisha kuwa waathirika hao bado wanauhitaji wa misaada hivyo amewaomba wadau wengine kujitokeza kusaidia waathirika wa mafuriko hayo.
Naye Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati Bi. Janeth shango kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa benki hiyo ametoa pole kwa wananchi waliyoathirika Wilayani Kilosa ambapo benki hiyo imetoa shilingi milioni 10.
Bi.Janeth amebainisha kuwa Benk hiyo ina utaratibu wa kutoa kwa wananchi sehemu ya faida wanayoipata hususan kwa waliopatwa na matatizo mbalimbali ili kuungana na Serikali katika kupunguza matatizo kwa wananchi hao.
Akizungumza kwa niaba ya chama cha mapinduzi mkoani humo, Katibu wa Chama hicho ndg. Solomon Kasaba amemshukuru Mkuu wa Mkoa huo na Mkuu wa wilaya ya Kilosa na Kamati za Ulinzi na Usalama pamoja na wadau waliojitokeza kutoa misaada kwa waathirika wa mafuriko wilayani kilosa na akatumia fursa hiyo kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kutoa misaada kwani bado uhitaji ni mkubwa.
Misaada iliyotolewa kwa waathirika wa mafuriko Wilayani Kilosa ni pamoja na vifaa vya ndani kama sufuria, ndoo, masinia mashuka, sahani na bakuli. Vingine ni vyakula kama mchele, unga wa sembe, mafuta ya kupikia, maharagwe na sukari.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.