Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amewataka wadau wa mazingira kuunga mkono kampeni mbalimbali zinazolenga utunzaji wa mazingira katika Mkoa huo ili kutapunguza uharibifu wa mazingira.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza na wadau wa mazingira wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Mhe. Adam Malima ametoa kauli hiyo Juni 14 mwaka huu wakati wa hafla ya uzinduzi wa kampeni ya uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyofanyika katika viwanja vya chuo cha ualimu Morogoro katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema uharibifu wa mazingira uliokithiri Mkoani humo ni pamoja na uchomaji moto misitu, ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa na kuni na kueleza kuwa ni wakati sahihi kulichukulia jambo hilo kwa uzito na kuwataka wadau hao kuunga mkono kampeni za utunzaji wa mazingira ili kuondoa athari zitokanazo na uharibifu huo.
"...kwa hiyo mimi nawaomba sana wadau wa mazingira msipindishe maneno kwenye hili...kuzungumzia suala la ukataji miti, uharibifu wa misitu ni kama kumpa mtoto krolokwini mpatie chungu, kali lakini badae tutakuja kuelewana tu..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima anapanda mti katika eneo la chuo cha ualimu Morogoro.
Aidha, ameongeza kuwa mito inayopita ndani ya Mkoa huo inachangia uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Kihansi Megawati 180, Kidatu Megawati 204 na bwawa la Mwalimu Nyerere zaidi ya megawati 2,000 na kupelekea Mkoa utachangia kwa 80% ya nishati ya umeme unaozalishwa hapa nchini baada ya Bwawa la Mwl. Nyerere kukamilika.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro wakipanda miti kwenye eneo la chuo Cha ualimu Morogoro wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utunzaji wa mazingira.
Naye Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Limited Bi. Bhoke Angela amebainisha lengo la kuwakutanisha wadau hao wa mazingira ni ufunguzi wa kampeni ya uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi na salama Mkoani Morogoro.
Hapa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima anapokea mtungi wa gesi kutoka kwa wafanyakazi wa kampuni ya Taifa Gesi.
Mhe. Adam Malima akigawa mitungi ya gesi kwa Wahe. Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro.
kwa upande wake Mkuu wa chuo cha ualimu cha Morogoro Bw. Augustine Sahili amesema matumizi ya gesi yana faida sio tu kwenye mazingira bali hata katika kupunguza matumizi ya mkaa na kubainisha kuwa chuo hicho kabla ya kuanza kutumia gesi kilikuwa kinatumia zaidi ya Tsh.4,500,000 kwa mwezi kununua mkaa, lakini tangu kianze kutumia gesi kinatumia Tsh. 3,000,000 pekee, hivyo kuokoa zaidi ya Tsh. 15 milioni kwa mwaka.
Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Misitu Tanzania - TFS kanda ya Mashariki Bi. Patricia Manonga amesema Kanda ya Mashariki ina jumla ya misitu 80 ya hifadhi na kubainisha kuwa changamoto kubwa katika hifadhi hizo ni ukataji wa miti ambapo takribani hekta 400,000 zimekatwa.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa kampeni ya uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi na salama, jumla ya mitungi 300 ya gesi imegawanywa kwa wadau mbalimbali walioshiriki hafla hiyo na zoezi hilo la ugawaji wa mitungi ya gesi ni endelevu.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akigawa mitungi ya gesi kwa baadhi ya washiriki wa hafla hiyo ikiwa ni ishara ya kuzindua kampeni ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.