Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT – MMMAM) katika jamii unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa Rasilimali watu na fedha, hivyo kufanya kasi ya usambazaji wa uelewa wa programu hiyo kusuasua, hivyo wadau wa maendeleo hususan Sekta binafsi wameombwa kuchangia katika utekelezaji wa programu hiyo.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Rasilimali watu na Utawala Bw. Herman Tesha akizungumza na wadau wa maendeleo wakati akifungua kikao kazi cha siku moja cha wadau wa malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto.
Hayo yamebainishwa Septemba 06 mwaka huu na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Rasilimali watu na Utawala Bw. Herman Tesha wakati akifungua kikao kazi cha siku moja cha wadau wa malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Bw. Tesha amesema pamoja na serikali kufanya jitihada za kuiendeleza programu hiyo lakini bado kunachangamoto ya rasilimali watu na fedha hivyo wadau wa maendeleo wanamchango mkubwa katika kuhakikisha kuwa jamii inapata uelewa wa kutosha, hivyo amewaomba wadau hao kuchangia katika utatuzi wa changamoto hizo.
“...lakini niwaombe sana wadau wote ambao tumeshiriki hapa na wale ambao hawapo hapa kuendelea kuchangia kwa hali na mali kwenye utekelezaji wa programu hii...” amesema Bw. Tesha.
Katika hatua nyingine, Katibu Tawala huyo amebainisha kuwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imeonesha asilimia 30 ya watoto Mkoani humo wanaudumavu, asilimia 10 wanauzito pungufu na asilimia 3.9 wanaukondefu hivyo jamii imeshauriwa kupitia programu hiyo kuzingatia lishe bora.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Rasilimali watu na Utawala Bw. Herman Tesha akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa maendeleo baada ya ufunguzi wa kikao kazi cha siku moja cha wadau wa malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuweka msukumo katika utekelezaji wa programu hiyo ikiwemo kuboresha huduma za afya hususan za mama na mtoto pamoja na kuboresha sekta ya elimu kuanzia ngazi ya awali kwa kujenga madarasa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Childhood Development Organization Bi. Felistas Kalomo amewasisitiza wadau hao kuchangia utekelezaji wa programu hiyo ili kupata matokeo chanya yanayotarajiwa.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Childhood Development Organization Bi. Felistas Kalomo akisisitiza wadau wa maendeleo kuchangia utekelezaji wa programu ya MMMAM.
Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT – MMMAM) imelenga kuhamasisha Afya bora kwa mama na mtoto, lishe bora, malezi yenye muitikio, ulinzi na usalama wa mtoto pamoja na fursa za ujifunzaji kwa watoto walio kati ya miaka 0 hadi 8 na inatekelezwa ndani ya miaka mitano 2021 hadi 2026.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.