Kutokana na kuongezeka kwa matukuio ya ukatili kwa Watoto hapa nchini wadau wa maendeleo washauriwa kuongeza ushirikiano katika suala zima la malezi bora kwa Watoto kwa kuwa ndio Taifa la kesho.
Ushauri huo umetolewa Novemba 18, mwaka huu na Bi. Peris Lumambo Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero wakati akichangia hoja kwenye kikao cha mapitio ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto kilicho fanyika katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Afisa Ustawi wa Jamii amesema matukio ya ukatili dhidi ya Watoto yanaongezeka siku hadi siku hivyo ametoa wito kwa wadau, wazazi, Serikali na makundi yote katika jamii kuongeza nguvu katika malezi ya Watoto ili kujenga jamii yenye maadili mema.
“...wito wangu kwa sekta zote idara ya afya, ustawi wa jamii, lishe, elimu, maendeleo ya jamii lakini tukishirikiana na jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na watu wa Mahakama tushirikiane katika suala zima la malezi kwa sababu sasa hivi hali ni mbaya...” amesema Bi. Peris Lumambo.
Aidha, Bi. Peris Lumambo amesema kuwa matukio mengi ya ukatili kwa Watoto kama vile ulawiti, ubakaji na vitendo vingine vinafanywa na ndugu wa karibu, hivyo wazazi wanatakiwa kuwa karibu na Watoto wao ili kupunguza ukatili huo.
Sambamba na hilo Afisa Ustawi wa Jamii amewashauri wamiliki wa shule za Watoto wadogo ‘Day Care’ kuunda umoja wao na kupatiwa elimu ya malezi bora kwa Watoto ili kujenga jamii bora kwa kuwa wao muda mwingi wanakuwa na Watoto hao.
Kwa upande wake Bi. Felistas Kalomo Mkurugenzi Mkuu Shirika la Maendeleo ya Mtoto (CDO) amesema suala la malezi linawahusu wazazi wote wawili baba na mama ili kumjenga mtoto katika maadili yanayofaa katika jamii zetu, kulega lega kwa wazazi katika majukumu yao ya ulezi wa familia kunasababisha Watoto kuharibikiwa kimaadili, ameongeza kuwa wazazi wanawajibu wa kuangalia usalama wa watoto wao ili kubaini changamoto zinazo wakumba Watoto.
Akihitimisha kikao hicho Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio amesema kikao kijacho kunahaja ya kushirikisha wadau mbalimbali ambao kwa kiasi kikubwa wanahusika na suala la malezi na maadili kwa Watoto ili kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya ukatili kwa Watoto na kujenga malezi bora kwa jamii.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.