Wafanyabiashara ndogondogo kunufaika na vitambulisho vya kidijitali.
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuja na mfumo mpya wa kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo na kuwapatia vitambulisho vya kidijitali kwa lengo la kuwatambua, kupata takwimu sahihi na kuwapa mazingira rafiki ya kufanyia biashara wafanyabiashara hao.
Hayo yamebainishwa Februari 20, 2024 na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Neema Dachi wakati akifungua kikao cha mafunzo kwa Maafisa Biashara, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa TEHAMA kutoka Halmamshauri zote za Mkoa huo kilichofanyika ukumbi wa Chifu Kingalu uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akibainisha zaidi Bi. Neema Dachi ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Usimamizi wa Serikali za Mitaa ametaja faida watakazopata wafanyabiashara hao mara baada ya kujisajili na kupata vitambulisho hivyo vya kidijitali kuwa ni pamoja na Kutambulika na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kutambulika na Jeshi la Polisi pamoja na kutambulika kwenye Ofisi za Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri.
Aidha, Bi. Neema amesema vitambulisho hivyo ambavyo wafanya biashara ndogondogo wanahimizwa kuwa navyo vitawasaidia katika kutunza fedha na kufanya mihamala mbalimbali ya kifedha pamoja na kuunganishwa na mifuko ya kijamii kama vile NSSF.
“….Serikali imeamua kuja na mfumo wa kidijitali ili kuwatambua wafanya biashara ndogondogo na itawasaidia kufanya biashara zao pasipo kubugudhiwa….” amesema Bi. Neema.
Katika hatua nyingine Kaimu Katibu Tawala huyo wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wafanyabiashara ndogondogo kwa kutoa fedha kutoka Hamlashauri za Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya ujenzi wa maeneo ya kufanyia biashara zao.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya jamii kutoka Wizara ya Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bw. David Malebetho amewataka wafanyabiashara ndogondogo Mkoani humo kujitokeza kwa wingi na kujisajili ili kupata vitambulisho hivyo na kuondokana na changamoto zinazowakabili zikiwemo za kutofahamika na kutokuwa na maeneo sahihi na salama ya kufanyia biashara zao hivyo kupelekea kuzagaa katika maeneo mbalimbali bila mpangilio na kukosa uhuru wa kufanya biashara zao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.