Wafanyabiashara watakiwa kujiepusha na matumizi ya mifuko ya plastiki, watakaokaidi kufikishwa mahakamani.
Serikali Mkoani Morogoro imewaagiza Wadau na wananchi wote kujiepusha na matumizi ya mifuko ya plastiki pamoja na mifuko mbadala isiyokidhi ubora na viwango vilivyoainishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kwamba watakaokaidi agizo hilo watafikishwa Mahakamani.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa adhara uliofanyika nje ya soko kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Agizo hilo limetolewa Septemba 17 mwaka na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Aboubakar Mwassa alipotembelea soko la Chifu Kingalu lililoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo la kuwakumbusha wafanyabiasha kujiepusha na matumizi ya mifuko hiyo lakini pia kusikiliza kero za wafanyabiashara wa soko hilo.
Akibainisha kuhusu matumizi ya mifuko ya Plastiki, Fatma Mwassa amesema mojawapo ya vigezo vya mifuko inayoruhusiwa kutumika kwa mujibu wa TBS ni pamoja na mifuko hiyo iwe na anwani na jina la mzalishaji, iwe na alama za urejelezaji, iwe imethibitishwa ubora wake na TBS na iwe na unene usiopungua microns 30 kwa upande mmoja, au Microns 60 kwa pande zote mbili.
Mkuu wa Wilaya ya manispaa ya morogoro Albert Msando akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano.
Kwa upande wa mifuko mbadala mifuko hiyo iwe na jina na anwani ya mzalishaji, iwe na alama au maneno ya urejelezwaji iwe na uzito usiopungua gramu 70,ioneshe uwezo wake wa kubeba na ubora wake uwe umethibitishwa na TBS.
Kwa mujibu wa kanuni ya 8 kifungu kidogo A mpaka E ya kanuni za usimamizi wa mazingira za kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ya mwaka 2019,inaeleza kuwa mtu yeyote akikutwa anatumia mifuko ya plastiki isiyo na ubora na kukutwa na hatia anatakiwa kufikishwa mahakamani.
“mtu yeyote atakayeingiza au kusafirisha nje ya nchi au kuzalisha au kuuza au kuhifadhi au kusambaza au kumiliki au kutumia mifuko na vifungashio vya plastiki kinyume na kanuni, atakuwa ametenda kosa na endapo atatiwa hatiani kulingana na kosa anaweza kufikishwa mahakamani” amesema Fatma Mwassa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akizungumza na Wananchi waliohudhuria mkutano wa adhara
Agizo hilo la Fatma Mwassa la kutotumia mifuko ya plastiki na vifungashio visivyo na ubora linakuja ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Dkt Philip Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokomeza mifuiko hiyo isiyokuwa na ubora na kukumbushwa na Dkt. Suleman Jafo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira alipozungumza na waandishi wa habari Mjini Dodoma Agosti 26, 2022.
Meneja wa kanda Morogoro Rufiji NEMC Amina Kibola akitoa maelekezo ya madhara ya mifuko ya plastiki isiyokidhi viwango na ubora kwa wananchi
Katika hatua nyingine Fatma mwassa akiwa katika soko hilo ametatua baadhi ya kero za wananchi ikiwa ni pamoja na malalmiko ya ufujaji fedha za makusanyo katika soko hilo ambapo Mkuu huyo ameelekeza kuwa kuanzia sasa fedha zote zinazokusanywa katika soko hilo zilipwe kupitia Control number ili kudhibiti upotevu wa fedha hizo za Serikali.
Aidha, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ashirikiane na wataalamu wake kufanya upya uchaguzi wa Viongozi wa Soko hilo ili kupata viongozi wapya badala ya kubaki na viongozi wanaolalamikiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa akikagua Mabanda ya wamachinga soko kuu la Chifu Kingalu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro
Akipokea maagizo ya Mkuu wa MKoa, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amesema anakwenda kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na kiongozi wake huku akiahidi mbele yake kuwa uchaguzi wa viongozi wa Soko la Chifu Kingalu utafanyika kwa huru na haki.\
Akizungumzia kuhusu mifuko ya plastiki, Meneja wa Kanda ya Morogoro - NEMC Amina Kibola amewaasa watanzania kutumia mifuko ya vikapu badala ya mifuko ya plastiki kwa kuwa amesema mifuko hiyo ina madhara makubwa kwa binadamu, wanyama na udongo pamoja na kuharibu mazingira kwa kuwa mifuko hiyo haiozi na inakaa hadi miaka 500 ardhini jambo ambalo ni hatari kwa vizazi vya baadae.
Muonekano wa soko kuu la Chifu Kingalu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro
Kwa upande wao wananchi akiwemo Philip Msangi Mkazi wa Morogoro na mfanyabiashara wa soko la Chifu Kingalu yeye anapinga kubomolewa kwa vibanda vya biashara vilivyojengwa sokoni hapo kwa hoja kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika vibanda hivyo, anashauri kuweka barabara kila baada ya vibanda hivyo lengo kila mfanyabiashara aonekana lakini sio kuvibomoa vibanda vyote.
Kuhusu mifuko ya plastiki Bw. Msangi anasema kwa sasa kila mwananchi anajua kuwa mifuko ya plastiki imepigwa marufuku na Serikali na kila mmoja anajua athari zake na kwamba wanaoingiza au kutumia wanakaidi tu na kuiomba serikali iwachukulie hatua kali.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.