Wahandisi wa Ujenzi Mkoani Morogoro wamehimizwa kuwa waadilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa miradi inayolenga kuwahudumia watanzania kupitia fedha zinazotolewa na Serikali katika Halmashauri zao.
Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Utumishi na Utawala Mkoa wa Morogoro akiwa kwenye kikao kazi cha Sekta ya Ujenzi.
Ushauri huo umetolewa Oktoba 13 mwaka huu, na Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Utumishi na Utawala Mkoa wa Morogoro Bw. Herman Tesha wakati akifungua kikao kazi cha Sekta ya Ujenzi kilichowakutanisha Wahandisi wote wa Sekta hiyo kutoka Halmashauri zote Tisa za Mkoa huo.
Wahandisi wakiwa kwenye kikao kazi cha Sekta ya Ujenzi Mkoa wa Morogoro.
Bw. Tesha amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inatoa fedha nyingi ili ziweze kukamilisha miradi ya maendeleo ikilenga kuwahudumia wananchi Katika sekta za Afya, Elimu, Maji n.k, hivyo wahandisi wanatakiwa kusimamia miradi hiyo kwa Uadililifu, weredi na maarifa ya hali ya juu.
Aidha, amewataka wahandisi hao kuzingatia mambo Matano yatakayowasaidia kukuza taaluma zao.
Ameyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya utumishi wa Umma, uadilifu kwenye utumishi wao, bidii ya kazi na kutii Serikali iliyopo madarakani.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Mhandisi Ezron Kilamhama alitaja lengo la kikao hicho kuwa ni utaratibu wao Kila mwaka kukutana wahandisi wote wanaofanya kazi ndani ya Mkoa huo ili kujadili changamoto mbalimbali za kiuhandisi, kubadilishana uzoefu na kukumbushana miongozo ya ujenzi inayotolewa na serikali kupitia Wizara ya Ujenzi.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Miundombinu Mhandisi Ezron Kilamhama akiwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu kwenye Kikao kazi cha Sekta ya Ujenzi.
Kwa upande wao Wahandisi wa Halmashauri za Mkoa huo akiwemo Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Hamis Magati amesema mabadiliko ya bei za vifaa vya ujenzi ni moja ya changamoto kubwa inayosababisha miradi mingi ya maendeleo kutokamilika kwa wakati ingawa Serikali inajitahidi kutoa fedha kwa wakati.
Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Hamis Magati akichangia mada kwenye kikao kazi cha Sekta ya Ujenzi.
Aidha ameongeza kuwa Halmashauri hiyo imepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 1, Milioni 180 kwa ajiri ya ujenzi wa madarasa katika shule za sekondari katika mji huo, pia amesema miradi hiyo imetakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi miwili, hivyo Halmashauri imejipanga kukamilisha miradi hiyo kwa haraka.
Nae Msanifu Majengo Mwandamizi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Baraka Lorila amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Madarasa katika Wilaya hiyo.
Sambamba na hilo amemshukuru pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Kilosa Bwana Kisena Mabuba kwa kuona umuhimu wa miradi hiyo na hivyo kununua gari ambalo litawasaidia kwa kiasi kikubwa katika ufuatiliaji na usimamizi wa Ujenzi wa miradi ya maendeleo Wilayani humo.
Wahandisi Sekta ya Ujenzi Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kikao kazi cha Sekta hiyo.
Kikao hicho kililenga kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo ya ujenzi, kutoa tathmini ya miradi iliyoanzishwa, kutoa maelekezo na mwongozo juu ya namna bora ya utekelezaji wa miradi kwenye Halmashauri za Mkoa huo ili ilete tija kwenye Mkoa na Taifa kwa ujumla na miradi inayotekelezwa iweze kuwa na ubora unaolingana na fedha zinazotolewa na Serikali yaani Value for Money.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.