Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na Kamati za Maafa za Mkoa na Wilaya ya Kilosa itatoa msaada wa chakula, magodoro, mashuka na mavazi kwa wahanga wa mafuriko yaliyotokea usiku wa kuamkia Disemba 5 mwaka huu na kusababisha kifo cha mtu mmoja huku baadhi ya familia zikikosa mahali pa kuishi.
Mhe. Malima amebainisha hayo Disemba 6 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Rudewa na Mvumi Wilayani Kilosa kwenye ziara yake ya kutoa pole kwa wahanga na kuangalia maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo.
Mhe. Malima ametoa pole kwa familia iliyoondokewa na mpendwa wao pamoja na wahanga waliopoteza makazi yao kutokana na mafuriko hayo huku akibainisha kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na kamati ya Maafa ya Wilaya ya Kilosa itatoa msaada huo vikiwemo vyakula na mahitaji muhimu.
"...nimekuja kuwaona ndugu zangu wa Mvumi na Rudewa baada ya janga ambalo limetukuta jana lakini jambo kubwa ni kupeana pole kwa niaba ya Dkt. Samia na Serikali yake lakini Kwa hatua ya kwanza kwa wale waathirika tuone tunafanya nini..." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu wa huyo wa Mkoa amewaagiza Mameneja wa Wakala ya Barabara Vijijini - TARURA, Shirika la Umeme - TANESCO na Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Mkoani humo kufanya tathmini na maboresho ya miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko hayo ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma za umeme, maji na Barabara kama ilivyokuwa awali.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amewataka baadhi ya watu kuacha tabia ya kuwaibia wengine pindi maafa yanapotokea huku akisema kuwa Serikali itawachukulia hatua za kisheria wale wote waliojihusisha na wizi wa mali wakati wa zoezi la uokoaji likiendelea ambapo watu watatu wanashikiriwa na Jeshi la Polisi Wilayani hapo kwa kuiba mali za wahanga wa mafuriko.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Shaka Hamdu Shaka amesema Jeshi la Polisi Wilayani hapo limejiandaa kukomesha vitendo vyote vya kiharifu ambapo kwa sasa Jeshi hilo linaendesha Kampeni ya kutokomeza uharifu na madawa ya kulevya, hivyo halitafumbia macho viashiria vyovyote vya uharifu na uvunjifu wa amani Wilayani humo na kuahidi kuwa Jeshi litahakikisha kuwa waliohusika na wizi wakati wa maafa wanachukuliwa hatua za kisheria.
Nao baadhi ya Wahanga wa Mafuriko hayo akiwemo Bw. Mohammed Twahibu ambaye nyumba yake imesombwa na maji amesema chanzo cha maji kuzingira nyumba za watu ni kukosekana kwa tuta la kuzuia maji kuingia kwenye makazi ya watu, hivyo ameiomba serikali kufanya maboresho ya kingo za mto Mvumi ili kuepusha athari zaidi kwa siku zijazo.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ametembelea maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo hususan Vijiji vya Rudewa na Mvumi na kuzungumza na wananchi na kuwataka kuwa watulivu wakati huu, huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini zaidi na kutoa wito kwao kuendelea kuchukua tahadhari za mvua zinazoendelea kunyesha hapa mkoani.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.