Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo kwa kushirikiana na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaoiba na kuharibu miundombinu ya barabara ikiwemo alama za barabarani na vyuma vya madaraja kwa kuwa amesema kufanya hivyo ni moja ya kosa la uhujumu uchumi wa nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (kulia) akizungumza wakati kikao na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa pamoja na wadau wa sekta ya mifugo kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega.
Mhe. Adam Malima ametoa kauli hiyo Julai 3 mwaka huu wakati wa kikao na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa pamoja na sekretarieti ya Mkoa na wadau wa sekta ya mifugo, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdalah Ulega (kushoto) akisisitiza jambo wakati wa kikao, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Serikali inatoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi ya miundombinu ikiwemo ya barabara lakini watu wachache wasio na nia njema na Serikali kwa makusudi wanaharibu na kuiba alama za barabarani, na kuharibu kingo za madaraja, hivyo amesema tabia hiyo haikubaliki na kuitaka kamati ya ulinzi na usalama hiyo pamoja na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro kuwachukulia hatua Kali za kisheria wale wote wanaojihusisha na tabia hiyo.
"...Serikali inachukua pesa, inakopa pesa, inakata kwenye makodi, inachukua kwenye road funds, inaenda kutengeneza barabara, watu kwa makusudi...huu ni wito kwa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa..." Amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Adam Malima amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo ACP Hassan Omary kuwasilisha taarifa ya hatua zilizochukuliwa ndani ya siku Saba ikiambatana na taarifa za kukamatwa kwa mtandao unaohusika na uharibifu huo.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amewataka viongozi wa Mkoa huo kushirikiana ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vinakomeshwa ili barabara za Mkoa huo ziwe salama.
Hawa ni baadhi ya wahe. Wakuu wa Wilaya za Mkoa wakiwa kwenye kikao.
Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema tathmini ya uharibifu huo imefanyika ambapo jumla ya mita 268 katika maeneo ya Magubike, Mtumbatu na Mkwambe uharibifu huo umefanyika sawa na shilingi 46,900,000 ya gharama hiyo inatokana na vyuma vya madaraja, alama za barabarani 72 zimeondolewa katika barabara ya Dumila - Ludewa - Kilosa.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe Kyamba akitoa tathmini ya uharibifu wa miundombinu ya barabara uliofanyika.
Sambamba na taarifa hiyo, Mhandisi Kyamba ameongeza kuwa kwa kushirikiana na vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama likiwemo jeshi la Polisi baadhi ya watuhumiwa wa sakata hilo wamekwisha kamatwa.
Naye Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Hassan Omary ametoa wito kwa wananchi na kutoa Uelewa kuwa vyuma hivyo ni mali ya Serikali, hivyo kuvichukua ni kuhujumu uchumi na ni kosa kisheria.
Huyu ni Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ACP Hassan Omary.
Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa huo kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi na viongozi wa maeneo yao wanapoishi ili kukabiliana na uharifu huo.
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu Mhandisi Ezron Kilamhama (kushoto) akiwana Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Ndg. Solomon Kasaba.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.