Wahasibu wa Halmashauri za Serikali za Mitaa Mkoani Morogoro wametakiwa kufanya kazi kwa kufuata Sheria, Taratibu, Kanuni, Maadili ya kazi zao ili kuepuka kupoteza nafasi hizo kwa kwenda kinyume na maadili ya kazi zao ikiwa ni pamoja na kutoa nywila za mfumo wa malipo Serikalini - MUSE.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo alipokuwa akifungua mafunzo ya mfumo wa Malipo Serikalini - MUSE kwa Wahasibu wa Halmashauri, maafisa Manunuzi na Maafisa TEHAMA yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki hii katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mhandisi Kalobelo amewataka na kuwaonya wahasibu katika kikao hicho kutothubutu kutoa nywila za mfumo huo kwa mtu asiyehusika kwani kufanya hivyo ni kukiuka maadili na sheria za kiutumishi na atakaebainika atakuwa sehemu ya uharifu pindi itakapobainika kuna tatizo kwenye mfumo huo katika ya Ofisi yake.
‘’Nisisitize kwa waweka hazina, kumekuwepo na tabia kwamba password unazopewa unagawa kwa mtu mwingine ambaye hana ethics za kutumia huo mfumo, wewe umefundishwa na unajua madhara ya kutoa password kwa mtu mwingine, sasa nawaomba hizo password mtakazopewa ziwe zako mwenyewe kwa majukumu yako’’ alisisitiza Mhandisi Kalobelo.
Sambamba na hayo, Mhandisi Kalobelo amewataka washiriki wa kikao hicho kushiriki kikamilifu kwa kuwa watulivu, wasikivu na wavumilivu ili kujengeana uelewa na kufanyakazi kwa vitendo katika mafunzo hayo.
Akibainisha umuhimu wa matumizi ya mfumo wa MUSE, Afisa Hesabu kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI Idara ya TEHAMA Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Fedha Bi. Catherin Uyoga amesema lengo la kikao hicho ni kuwajengea uwezo wahasibu wa Halmashauri, Maafisa TEHAMA na Maafisa Ununuzi ili ifikapo Julai mwaka huu Halmashauri zote Tanzania zianze kutumia mfumo huo, hivyo kuwawezesha kufanya malipo ya fedha za Serikali na malipo mengine kwa wananchi bila kukwama.
amesema MUSE imetengenezwa baada ya changamoto zilizojitokeza katika mifumo mingine ya Serikali kutokidhi mahitaji pamoja na kugharimu fedha nyingi katika kuitumia ukiwemo mfumo wa EPICA, kwa sababu ni mfumo kutoka nje ya nchi hivyo Serikali kuamua kuunda mfumo wa MUSE ambao tayari baadhi ya taasisi za Serikali zimekwisha anza kuutumia.
Naye, Afisa Msimamizi wa Fedha Mkuu kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro Bi. Flora Rajab amesema mfumo huo utawasaidia katika kusimamia Halmashauri za Mkoa huo lengo kuu ni kuziwezesha kufanya usuluhishi wa mahesabu ya fedha kila mwezi, uchukuaji wa masurufu, uandaaji wa taarifa za mwezi, utoaji wa taarifa za robo mwaka na taarifa za mwisho wa mwaka kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Margareth Nembo amesema MUSE imetengenezwa baada ya kutokea changamoto nyingi ndani ya mifumo iliyokuwepo kwani mfumo wa MUSE ni mzuri kutokana na kutotumia gharama kubwa ukilinganisha na mfumo wa EPICA kutoka nje ya nchi hivyo kutumia ghalama kubwa wakati wa uendeshaji.
Mfumo wa Malipo Serikalini yaani MUSE ulianza kubuniwa na Wizara ya Fedha na Mipango na kuundwa kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI baada ya kufanya uchambuzi wa matumizi ya mifumo ukiwemo EPICA na kubaini kuwa Serikali ilikuwa inatumia fedha nyingi sana kugharimia ununuzi, uundaji usimikaji na uendeshaji wa mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha za Umma na kuamua kuchukua hatua ya kuunda mfumo huu mpya wa MUSE hapo Machi, 2019.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.