WAHUDUMU WA MABASI NCHINI KUTAMBULIWA RASMI NA SERIKALI.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Nsemwa amesema Serikali kupitia chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa kushirikiana na Mamlaka ya udhibiti na usafiri wa ardhini (LATRA) Wameanza kuwatambua rasmi watoa huduma za mabasi ya masafa marefu na mijini kwa kuwapatia mafunzo yatakayowasaidia kuongeza weledi katika utendaji kazi ndani ya sekta hiyo ya usafirishaji.
Mhe. Rebecca ameyasema hayo Machi 18, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku tano katika ukumbi wa mikutano za Ofisi ya TAFORI zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na kubinisha kuwa Wizara ya Uchukuzi na Wizara Elimu Sayansi na Teknolojia waliwezesha kuwepo mradi wa East Afrika Skills for Transportation and Regional Intergration Project ambapo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (World Bank) lengo ni kuwafanya watoa huduma ya mabasi kutambulika na Serikali.
“…Ndugu zangu nimefurahi sana kwa kujali kada hii ya uhudumu wa mabasi ya masafa marefu na mjini kwa kurasimisha kada hii kuwa kada inayotambulika na Serikali….” Amesema Rebecca Nsemwa.
Pia Mkuu huyo wa Wilaya amekipongeza Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Malaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini(LATRA) kwa kufikia hatua ya kutoa mafunzo kwa Wahudumu wa mabasi ambapo itawasaidia kutoa huduma bora kwa kuzingatia sheria na taratibu zote za utoaji huduma.
Katika hatua nyingine Mhe. Rebeca Nsemwa ametoa wito kwa viongozi wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa weledi ili kukifanya chuo hicho kuwa mahala sahihi pakupatia mafunzo mbalimbali.
Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) anayeshughulikia Utawala na fedha Bi.Zainabu Mshana amesema mafunzo hayo yataongeza hali ya usalama wa abiria na mali zao na kwamba yatakua ni endelevu, hivyo amewataka watu kuchangamkia fursa ili kujitokeza kwa wingi kujiunga na Chuo hicho katika Taamula hiyo ya Uhudumu wa Mabasi.
Naye Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Udhiti na Usafiri Ardhini (LATRA) Bw.Andrew Mlacha amebainisha kuwa kupitia mafunzo yanayotolewa watapata takwimu sahihi zitakazowawezesha kuwatambua rasmi watoaji huduma katika mabasi ya masafa marefu na mijini.
Naye Filbert Othman akiongea kwa niaba ya wenzake wanaopata elimu hiyo ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali na kuweza kuwapatia elimu ambayo ni muhimu na itawasaidia kutambulika na kupata haki zao kama wafanya kazi wengine.
Mafunzo hayo ya siku tano, tayari yametolewa katika baadhi ya Mikoa ikiwemo Kilimanjaro, Mbeya na kwa sasa yanatolewa katika Mkoa wa Morogoro ambapo jumla ya washiriki 73 wamejitokeza kupata mafunzo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.