Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka waratibu wa wafanyabiashara ndogo pamoja na viongozi wa wafanyabiashara kuendelea kuwahamasisha wafanyabiashara hao kujisajili katika mfumo wa kielektroniki ili kupata vitambulisho vitakavyowatambulisha katika maeneo yao ya kazi.
Mhe. Malima amesema hayo Disemba 19, Mwaka huu wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho vya kielekroniki vya wafanyabiashara ndogo Mkoa wa Morogoro uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Akifafanua zaidi Mkuu huyo wa Mkoa amesema takwimu ya usajili wa wafanya biashara hao kujiandikisha ni 3042 kwa mkoa mzima na kwamba takwimu hiyo bado iko chini kwani amesema wafanya biashara ndogo ndogo wapo wengi zaidi ya waliojiandikisha hivyo ametaka juhudi ya uhamasishaji ifanyike ili wajisajiri wafanyabiashara wengi.
"... kwa hiyo leo katika biashara ndogo ndogo waliosajiliwa ni 3042 wanaume 1108 na wanawake ni 1934... tuendelee kuwahamasisha wajitokeze kwa wingi kujisajili..." amesema Mhe. Adam Kighoma Malima
Katika hatua nyingine, Mhe. Adam amewaagiza wenyeviti wa Halmashauri kila kikao cha Baraza la Madiwani maafisa uratibu wawasilishe taarifa ya wafanyabiashara wanaondelea kujisajili pia amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kusaidia kuhamasisha na kusimamia ugawaji wa vitambulisho.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Morogoro Bw. Gibson Mathew ambaye pia ni Mratibu wa Wafanyabiashara ndogo ndogo Mkoani humo amesema vitambulisho vilivyotolewa vitawapa wafanyabiashara hao fursa ya kukopa banki ya NMB ambayo ndiyo imeingia mkataba na serikali ili kuweza kuongeza mitaji yao katika utendaji kazi wao.
Kwa niaba ya wafanyabiashara ndogo ndogo Mwenyekiti wa machinga Mkoani wa Morogoro Bw. Faustine Francis amesema amefurahi kutambuliwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupewa vitambulisho ambapo ndio utambulisho maalum katika maeneo yao ya kazi ili kufanya shughuli zao bila bughudha.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.