Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Gairo kuhakikisha wanaitumia nafasi waliyopewa na kuitendea haki kwa kutoa huduma bora kwa wananchi kwa maendeleo ya wanagairo, Mkoa na Tanzania kwa ujumla.
Mhe. Malima amesema hayo Oktoba 12, 2024 wakati wa hafla fupi ya kuzindua Baraza la ardhi na nyumba na kuwaapisha wajumbe wa Baraza hilo, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wajumbe hao kuhakikisha wanaitumia nafasi hiyo kutoa haki kwa usawa na kwa uadilifu katika utekelezaji wa majukumu kwani dhamana waliopewa ni kwa ajili ya manufaa ya wengi na kuwatumikia wananchi wa Wilaya hiyo, hivyo wanapaswa kufuata taratibu na vigezo vyote vya Baraza hilo.
"...wajumbe tuliowaapisha leo kwanza mmepewa dhamana kubwa, naomba muitumie nafasi hiyo na kuiona kama ni heshima kubwa na jambo kubwa, matarajio yangu mtaenda kuitendea haki nafasi mliopewa kwa uadilifu mkubwa..." amesema Mhe. Adam Malima.
Mhe. Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wanagairo na kuhakikisha Wilaya hiyo inapata huduma za taasisi mbalimbali za utoaji haki zikiwemo mahakama, magereza, Ofisi ya Baraza la ardhi na Ofisi ya mwendesha mashtaka ambazo hapo awali wananchi walitembea umbali mrefu kuzifuata huduma hizo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.