Wajumbe wa bodi ya barabara Mkoa wa Morogoro wameazimia kwa kauli moja kuwasilisha maombi ya kuongezewa bajeti kwa ajili ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROARDS) na Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoani humo ili kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya barabara ndani ya mkoa huo.
Wajumbe wa Bodi hiyo wameazimia hilo Machi 4, Mwaka huu wakati wa kikao cha 43 cha bodi ya barabara kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Magadu uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro hoja iliyotokana na ukweli kwamba Mkoa huo ni mkubwa ukilinganisha na mikoa mingi hapa nchini.
Akifafanua zaidi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa huo ni mkubwa huku akitolea mfano kutoka mpakani mwa Namtumbo hadi Gairo ni umbali wa km 800 ukiwa bado ndani ya mkoa hivyo hauwezi kuwa na bajeti sawa na Mikoa mingine kwa sababu ya ukubwa huo.
"...tumejenga hoja TANROARDS na TARURA kwamba Mkoa wa Morogoro muuangalie kwa utofauti... hebu angalia kutoka Namtumbo hadi Gairo ni km 800 halafu bajeti inafanana na Mikoa mingine lazima watuangalie..." Amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amekemea vikali mwananchi aliyeharibu barabara kwa kulima zao la mpunga sehemu ya kipande cha barabara na kuleta taharuki kwa wananchi wengine na kuharibu barabara hiyo hivyo amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro kushughulikia haraka kadhia hiyo kabla ya Machi 8, Mwaka huu ili siku ya tarehe hiyo atakapotembelea asikute uharibifu huo na hatua ziwe zimechukuliwa kwa mhusika.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka TANROARDS na TARURA kuweka alama za barabarani kwa maeneo yote yanayostahili kuwekewa alama ili kusaidia usalama kwa wasafiri na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali yakiwemo mazao.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROARDS Mkoa wa Morogoro Mhandisi John Mkumbo amesema TANROARDS inasimamia barabara zenye urefu wa km 6406.69 kati ya hizo km 100.07 ni za kiwango cha lami, km 1487.3 ni za changarawe na km 4,819.28 ni za udongo.
Amesema miradi hiyo ya maendeleo inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa kiwango cha lami kwa kipande cha Ifakara - Taweta - Madeke, ujenzi wa daraja la duthumi ( barabara ya bigwa kisaki), ujenzi wa kiwango cha lami Gairo Pr. school njia panda ya malimbika hospitali, ujenzi wa kiwango cha lami eneo la chuo cha mzumbe barabara ya Sangasanga - langali utekelezaji unaendelea, na ukarabati wa barabara ya Mvomero - Ndole - Kibati pia utekelezaji unaendelea.
Naye, Meneja wa Wakala ya Barabara ya Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Emmanuel Ndyamkama amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 TARURA Mkoani humo imepanga kutumia kiasi cha Tsh. Bil. 24.9 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara kwa kupitia vyanzo vya fedha za mfuko wa barabara, mfuko wa jimbo na fedha za tozo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.