Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema wakadiliaji majenzi wamekuwa nguzo katika utoaji wa thamani ya miundombinu mbalimbali ikiwemo miradi ya barabara, maji, elimu na afya ili kukadiria miradi hiyo kabla ya kuanza ujenzi ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha za Serikali.
Mhe. Malima amesema hayo Oktoba 10, Mwaka huu kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa (MB) katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa 30 wa wakadiliaji majengo na semina ya mafunzo kwa wataalam wa ujenzi ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo maafisa ukadiliaji hao.
Akifafanua zaidi, Mhe. Malima amesema wakadiliaji majenzi ndio wanapaswa kufanya makadirio ya miradi ili kuwa na miradi itakayolingana na fedha zitakazotolewa (value for money) na kuondoa changamoto ya kumalizika fedha kabla mradi kuisha.
"... ninyi mnaona suala la ujenzi mimi naona suala la kiuchumi kwenye value for money kwamba msipofanya kazi yenu hakuna value for money... " amesema Mhe. Adam Kighoma Malima
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakadiliaji majenzi kujiimarisha katika matumizi ya teknolojia kwa kuongeza elimu na maarifa ili kuendana na wakati uliopo kwani teknolojia mpya zitafanya kupata miundo ya majengo mbalimbali ya kisasa.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wakadiliaji Majenzi cha Tanzania Qs. Bernard Ndakidemi amesema mwaka 2023/2024 Serikali imeajiri wakadiliaji majenzi 200 katika taasisi za ujenzi na kuiomba Serikali kupitia Wizara ya ujenzi kuwashirikisha wakadiliaji majenzi katika miundombinu ili kupata thamani halisi ya miradi na kuepuka upotevu wa fedha za umma.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma na Ufundi wa Umeme kutoka Wizara ya Ujenzi Qs. Mwanahamisi Kitogo amesema Serikali kupitia Wizara ya ujenzi imefanikiwa kufanya marekebisho ya usajili wa wabunifu majengo na wakadiliaji majenzi kuingia katika mfumo wa ajira Serikalini kwani mabadiliko hayo yamelenga kuongeza utendaji kazi wa kitaalamu katika miradi ya umma.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.