Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka Wakaguzi wa Ndani Mkoani humo kutokuwa na huruma katika utendaji kazi wao hususan wanapofanya ukaguzi wa fedha na miradi ya maendeleo katika maeneo yao kwa kuwa wao ndio jicho la Serikali.
Dkt. Mussa ameyasema hayo Machi Mosi, 2024 wakati akifunga Kikao Kazi cha Wakaguzi wa ndani wa Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa.
Katibu Tawala huyo ameeleza kuwa Wakaguzi wa ndani hususan wa Halmashauri wamekuwa wakifumbia macho ubadhilifu wa fedha unaofanyika kwenye Halmashauri huku akibainisha kuwa hali hiyo inasababisha miradi ya maendeleo kutekelezwa chini ya kiwango ama kutokamilika kwa wakati.
Kwa sababu hiyo Dkt. Mussa amewataka watendaji hao kutokuwa na aibu linapokuja suala la kusimamia ukusanyaji wa mapato kupitia mashine za PoS na kuwataka kutoa taarifa kwa ngazi husika ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa - TAKUKURU pindi wanapobaini kuwepo viashiria vya wizi wa fedha au vifaa vya miradi.
"...katika utendaji wetu wa kazi tunaoa aibu, tunaona muhali kutekeleza ule wajibu wetu wa kazi tuliopewa na hatimae mambo yanaharibika..."
Aidha, amewataka Wakaguzi hao kuhakikisha kuwa fedha zinazokusanywa zinapelekwa benki ili kuepusha wizi unaoweza kutokea.
Katika hatua nyingine Dkt. Mussa amewasisitiza Wakaguzi hao kujijengea utamaduni wa kukagua miradi ya maendeleo ili kujiridhisha matumizi ya fedha na ubora wa miradi hiyo inayotekelezwa katika Halmashauri zao kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza ubora wa miradi hiyo na kuwz na thamani ya fedha zilizotolewa.
Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi Bi. Neema Dachi amesema kikao kazi hicho kimelenga kuwakumbusha Wakaguzi wa Ndani majukumu yao ya msingi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kwenye ukaguzi wa fedha na miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakaguzi wa Ndani Mkoa wa Morogoro Bw. Isaac Mwang'onda kwa niaba ya Wakaguzi waliohudhuria kikao hicho amemshukuru Katibu Tawala huyo pamoja na timu yake kwa kuandaa kikao kazi hicho na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi maagizo na maelekezo aliyoyatoa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.