Wakazi 329,770 Mkoani Morogoro wanatarajia kupewa vitambulisho vyao vya Taifa kuanzia Novemba 22 mwaka huu kupitia Watendaji wa Kata katika maeneo wanayoishi ili kuondoa kilio cha kukosa vitambulisho hivyo na kuwakosesha haki yao ya kimsingi kwa muda mrefu.
Taarifa hiyo njema kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro imetolewa Novemba 11 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akipokea Vitambulisho hivyo kutoka kwa Afisa Usajiri wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Mkoa wa Morogoro Bw. James Malimo, tukio lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Mh. Malima amesema zoezi hilo la ugawaji wa vitambulisho hivyo linafanyika kwa awamu ya pili ambapo wakazi 329,770 wa Mkoa huo wataanza kupata vitambulisho vyao Novemba 22 mwaka huu ambapo awamu ya kwanza wakazi 677,588 walipewa vitambulisho hivyo mkoani humo.
“...leo hapa tunasema wananchi wote walioko Morogoro asilimia 94 sasa wanapata vitambulisho vyao halisia, ni jambo zuri sana...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo kuratibu vizuri na kusimamia zoezi nzimz la ugawaji wa vitambulisho hivyo katika Wilaya zao na kwamba hataki kusikia wananchi wakisumbuliwa wakati wa zoezi hilo.
Sambamba na hilo, Mhe. Adam Malima amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia vitambulisho hivyo, na kwamba anaamini wananchi Mkoani humo watafurahia kupatiwa vitambulisho hivyo kwa sababu vitaondoa changamoto iliyodumu kwa muda mrefu.
Mhe. Adam Malima amewasisitiza wananchi wa Mkoa huo waliokidhi vigezo vya kupewa vitambulisho hivyo, kuwa zoezi la ujisajili kwa ajili ya kupata vitambulisho bado linaendelea katika Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa na kuwataka wale wote ambao hawana wajitokeze kwa ajiri ya kujisajili.
Akikili kupokea maagizo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Judith Nguli amesema upatikanaji wa vitambulisho hivyo umejibu maswali ya muda mrefu kutoka kwa Wananchi wao, hivyo Wakuu hao wa Wilaya watafanyakazi kwa pamoja ili kutekeleza zoezi hilo katika Wilaya zao kama walivyoelekezwa na Mkuu wa Mkoa. Aidha, ametoa wito kwa Wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua vitambulisho vyao katika Ofisi za Watendaji wa Kata.
Naye, Afisa Usajili wa Vitambulisho vya Taifa Mkoa wa Morogoro Bw. James Malimo amesema awamu ya kwanza NIDA Mkoani humo ilitoa vitambulisho 677,588 kati ya 1,012,391 vilivyohitajika huku awamu hii inatarajia kutoa vitambulisho 329,770 sawa na asilimia 99 ya wakazi wa Mkoa huo watakuwa wamepewa vitambulisho vyao.
Aidha, ameongeza kuwa vitambulisho hivyo vitatolewa katika ofisi za Watendaji wa Kata katika Mkoa huo hivyo amewataka wanachi kufika katika ofisi hizo mara watakapopewa taarifa ili kuchukua vitambulisho vyao kuanzia Novemba 22 mwaka huu.
Kwa upande wake Afia Mtendaji wa Kata ya Tungi Bw. Masanja Laurent ameishukuru Serikali kwa kuleta vitambulisho hivyo ambapo sasa vitasaidia kupunguza kelele za wananchi kwa kuwa suala la vitambulisho kilikuwa ni kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro.
Vitambulisho hivyo vitagawanywa kwa wananchi wa Wilaya zote ambapo Wilaya ya Morogoro itapewa vitambulisho 159,613, Ulanga vitambulisho 974, Gairo 1950, Malinyi 1150, Kilosa 94,000 na Wilaya ya Kilombero itapokea 33,000.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.