Wakazi wa mji wa Kilosa wametafadharishwa kwa mara nyingine kuchukua hatua juu ya kuepukana na mafuriko yanayoendelea kuukumba mji huo kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha ndani na nje ya mji wa Kilosa na kusababisha athari kubwa ya miundombinu, makazi, vyakula na hata kugharimu maisha ya watu.
Wito huo umetolewa Leo Disemba 10, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe.Adam Kighoma Malima alipotembelea baadhi ya maeneo yaliyoathirika na mafuriko yaliotokea usiku wa kuamkia leo Disemba 10 katika Kata ya Mkwatani Mtaa wa Manzense B, Wilayani Kilosa Mkoani humo na kutoa pole kwa waathirika.
Mhe. Malima amebainisha kuwa ndani ya siku sita mfululizo, maeneo mbalimbali ya mji wa Kilosa yamepata athari ya mafuriko, maeneo hayo ni pamoja na Mvumi, Rudewa, Dumila, Kitete na maeneo ya Kilosa Mjini.
“…… Kitu tunachojua ni kwamba Kilosa yetu imekuwa kama bakuli, kwa hiyo maji yote yanayotoka huko milimani ukiongeza na maji yake yenyewe bado inabidi tukae kwa tahadhari kuhusu haya maafuriko….” amesema Adam Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo, kwa mara nyingine kufanya tathimini ya hasara ya jumla, kwa ajili ya kuangalia namna ya kutoa msaada wowote ule kwa waathirika wa mafuriko hayo ili waweze kujikimu.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amewataka Wanchi kuzingatia Sheria za Ujenzi wa makazi yao ikiwemo kupata vibali vya Ujenzi ili kuondokana na madhara ya maafuriko kwa kuwa watafahamishwa na wataalam sehemu sahihi za ujenzi wa nyumba za makazi yao.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD) Eng. Lazack Kyamba kurudisha haraka mawasiliano ya Daraja la mto Mkondoa linalo unganisha Kilosa na Mikumi ili wananchi wa mji huo na wasafiri wengine wanaotumia njia hiyo ili waweza kuendelea na shughuli zao za kawaida.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amewashukuru Wananchi wa Wilaya hiyo kwa kuonesha ushirikiano wa kutosha kila yalipotokea mafuriko hivyo kuepusha madhara ya Kibinadamu ambayo yangeweza kutokea.
Sambamba na shukra hizo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zaidi ya Shilingi Bilioni 13 kwa ajili ya ujenzi wa mitaro ya ya Barabara za Mjini Kilosa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.