Wakulima wa zao la mpunga katika vijiji vya Kigugu, Mkindo na Iyombo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro wamenufaika na kilimo cha zao hilo chini ya programu ya Farm To Market Alliance (FTMA) ambayo imewawezesha kulima kwa tija zao hilo.
Hayo yamesemwa Machi 22 mwaka huu na Mkurugenzi wa Taasisi ya Farm Afrika Bi. Marry Batman wakati wa ziara yake iliyolenga kujionea hatua iliyofikiwa na wakulima hao tangu kuanzishwa kwa programu ya FTMA hapa nchini.
Bi. Marry amefafanua kuwa lengo la program ya FTMA ni kumsaidia mkulima kukutana na mashirika ambayo yanatoa ushauri juu ya kilimo bora cha Zap la mpunga kwa kuwapatia elimu, zana bora za kilimo, pamoja na kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema wamekuja kuangalia mafanikio, na changamoto ambazo wakulima hao wanazipata kupitia programu hiyo ambapo vikundi mbalimbali vinavyozalisha zao la mpunga kupitia kilimo cha umwagiliaji, hivyo wamefurahishwa kuona wakulima wamepata mafanikio makubwa japokuwa kuna changamoto ndogo ambazo zikifanyiwa kazi zitaisha kabisa.
"...tumekuja kuangalia wanafanyaje kwenye hii programu na tumeona shamba darasa ambalo wamepanda aina tano za mpunga na hivyo itawasaidia kuchagua mbegu bora ambayo wanaweza kuitumia kwa msimu ujao wa kilimo..." amesema Bi. Marry.
Akitoa shukrani kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mradi huo kwa niaba ya wakulima wa Kijiji cha Mkindo Katibu wa Chama cha wakulima Bi. Khadija Rashid amesema kupitia mradi huo uzalishaji umeongezeka kwa sababu ya matumizi ya zana bora za kilimo ambazo wamezipata kupitia mradi huo.
Aidha, ameongeza kuwa mradi huo umewawezesha kupata soko la uhakika ambapo kampuni ya MW RICE MILLERS LTD ya Mkoani Morogoro inanunua mazao yao na kuwapatia wakulima hao mbegu bora zilizofanyiwa utafiti na TARI, DAWA na kupata elimu ya kilimo Chenye tija.
Hata hivyo, Katibu huyo amesema kupitia mradi huo umewawezesha kupata elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kulima kilimo shadidi ambacho kina tumia maji kidongo na mbegu kidogo lakini mavuno yake ni mengi.
Kwa upande wake Bw. Seifu Rashidi Abdalah ambaye ni mkulima katika skimu hiyo amemuomba Mkurugenzi wa FTMA kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi hivyo itawaongezea tija kwenye uzalishaji wa mpunga hii ni kutokana na kubadilika badilika kwa bei ya mpunga na mchele kwenye soko la dunia.
Mradi wa FTMA ulianzishwa kwa lengo la kumuwezesha mkulima kukuza kipato chake kwa kupata elimu, mbegu bora na zana za kisasa.
Mradi wa FTMA unafanya kazi katika nchi nne za Afrika ikiwemo Tanzania, Msumbiji, Rwanda na Kenya.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.