Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (MB) amewataka wakulima wa Wilaya ya Gairo na wakulima wote hapa nchini kujiunga na vyama vya ushirika kwa ajili ya kuinua uchumi katika familia zao na kwa ajili ya maslahi mapana ya sekta ya kilimo.
Naibu Waziri Silinde amesema hayo Oktoba 8, Mwaka huu wakati akifungua maonesho ya Samia Kilimo Biashara Expo 2024 msimu wa tatu yaliyofanyika Wilayani Gairo yakiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa wakulima ili kulima kilimo cha kisasa na cha kibiashara.
"... niombe na nitoe rai kwa wananchi wote wa Gairo kuendelea kujiunga na vyama vya ushirika na Watanzania wote katika maeneo yote nchini wajiunge na ushirika..." amesema Waziri.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema katika Wilaya ya Gairo kumekuwa na muitikio mkubwa ya wakulima kujiunga na vyama vya ushirika kwani mpaka sasa vyama vya ushirika 13 vimesajiliwa katika Wilaya hiyo, hivyo ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) kusajili vyama vingi Wilayani humo kwani amesema hiyo ni mojawapo ya kutatua changamoto ya masoko na pembejeo za kilimo.
Aidha, Naibu Waziri amewataka wakulima kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa mfumo huo unawasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa bei elekezi na iliyopo kwenye masoko hivyo kuongeza kipato chao.
Katika hatua nyingine ameipongeza Wizara ya Nishati kwa maonesho yao ya mfumo rafiki wa nishati safi ya kupikia yakiwemo majiko ya kupikia ikiwa ni kuunga mkono ajenda ya Mhe. Dkt. Samiaa Suluhu Hassan kwa maono ya kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo Gesi, umeme, mkaa mweupe na nyingine ili kuepuka uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.
Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote hapa nchini kuiga mfano wa Wilaya ya Gairo kuwa na maonesho ya Kilimo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wakulima, kulima kisasa zaidi na kuwaletea tija.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame amesema Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ameleta mageuzi katika sekta ya kilimo kutokana na uhitaji wa wakulima kwani zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania hapa nchini wanategemea kilimo, hivyo mageuzi hayo yamelenga kuondoa umasikini ndani ya jamii inayotegemea kilimo na ufugaji.
Naye, Naibu Mrajisi (Uhamasishaji) wa TCDC Bi.Consolata Kiluma amesema Tume hiyo itahakikisha inasajili vyama vingi vya Ushirika na kuvisimamia na kutumisa hiyo kutoa wito kwa wakulima kujiunga na vyama hivyo kwani lengo la vyama hivyo ni kukuza uchumi kwa wananchi.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.