Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kubainisha maeneo yenye uwezekano wa kuathiriwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu na kuweka mikakati ya kuudhibiti mapema hivyo kunusuru maisha ya watu.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Januari 17 mwaka huu kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa sasa hakuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ndani ya mkoa huo lakini Mkoa unaendelea kuchukua taadhari zote juu ya mlipuko wa ugonjwa huo huku akiwataka Wakurugenzi hao kushirikiana na wataalam wa afya kubainisha maeneo ambayo yako hatarini kupata ugonjwa huo hususan maeneo yenye mikusanyiko ya watu.
"...Pili nenda kaunde timu yako, nendeni mkaangalie maeneo ambayo yanaonekana kuwa ni hatarishi hayo ni maagizo yangu..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametaja baadhi ya maeneo yanayoweza kuathirika na ugonjwa huo kwa haraka kuwa ni pamoja na Manispaa ya Morogoro, Kilosa, Mikumi, na Ifakara kutokana na maeneo hayo kuwa na mwingiliano wa watu wengi hivyo amewataka wakurugenzi wa Halmashauri hizo wakishirikiana na wakazi wa maeneo hayo kuchukua taadhari kwa kufanya usafi katika masoko, vyoo vya stendi na maeneo mengine.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio ameeleza kuwa hadi kufikia Januari 17 mwaka huu hakuna taarifa yoyote iliyoripotiwa katika vituo vya Afya juu ya kuwepo kwa ugonjwa huo. Aidha, ameongeza kuwa Mkoa umepokokea vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa kipindupindu endapo kwa watabainika.
Nao Viongozi Dini akiwemo Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (K.K.K.T) Dayosisi ya Morogoro Askofu Jacob Mameo amewashauri Wanasiasa kuacha kabisa tabia ya kuwakingia kifua wananchi wanaofanyabiashara katika maeneo yaliyokithiri kwa uchafu hasa pale Watendaji wa Serikali wanapowaondoa wafanyabiashara katika maeneo hayo.
Amesema lengo la watendami hao wa serikali daima huwa linakuwa jema la kunusuru vifo vinavyoweza kutokana na mazingira hayo machafu, hivyo ni vema pande zote mbili zikawa na lengo moja la kutaka kuokoa maisha ya watu badala ya kuingiza siasa kwenye suala la maisha ya watu.
Kwa upande wake Mtaalam wa Epidemiolojia Mkoa wa Morogoro Dkt. Jonhas Masatu amebainisha njia za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kuwa ni pamoja na usafi wa mazingira na usalama wa chakula, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kusafisha vyoo wa mara kwa mara pamoja na kudhibiti mifumo ya maji taka.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.