Wakurugenzi watakiwa kuandaa mashamba darasa
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mikoa inayounda Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki wametakiwa kuandaa mashamba darasa ya vipando katika maeneo yao ili kuwawezesha wananchi ambao hawakushiriki maonesho hayo kujifunza kilimo cha kisasa kupitia vipando hivyo ili kilimo hicho kiwaletee mazao mengi na yenye tija.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani Ghaibu Lingo (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa mtaalamu baada ya kutembelea banda la maonesho la Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro
Witoa huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Pangani Ghaibu Lingo Mkoani Morogoro akiwa mgeni rasmi wa siku ya kwanza ya maonesho hayo ya wakulima na wafugaji maarufu kama Nanenane Kanda ya Mashariki inayoundwa na Mikoa minne ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Wenyeji Morogoro.
Ndugu Lingo amesema, kumekuwa na dhana kwa halmashauri nyingi kuandaa vipando kwenye mabanda yao kwa lengo la kufundishia na mashindano, lakini hawaweki mikakati ya kuandaa vipando hivyo kwenye halmashauri zao ili kutoa fursa ya kutoa elimu hiyo kwa wananchi waliokosa kushiriki maeneo ya Nanenane.
Kwa sababu hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya ya Pangani ametumia maonesho hayo kuwaagiza wakurugenzi wote wa kutoka mikoa hiyo kwenda kuandaa vipando hivyo mara watakaporejea katika maeneo yao kwa lengo la kupeleka elimu hiyo kwa wananchi waliobaki huko.
“Ni kweli Halmashauri nyingi wanaviandaa vipando kama sehemu ya kufundishia na mashaindano, lakini wanaporudi kwenye Halmashauri zao hawana maandalizi ya mkulima aliyekosa kujifunza kule kwenye nanenane ajifunze kwenye halmashauri zao” amesema.
“ ...nichukue nafasi hii kuwaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote wakirudi, waandae mashamba darasa ambayo yatawafanya wananchi waliokosa kujifunza kwenye nanenane wakajifunzie kule waliko” amesisitiza Bw. Lingo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya ya Pangani amewataka wananchi wa kutoka Mikoa hiyo na watanzania wote kwa jumla kuacha matumizi ya kilimo cha jembe la mkono, badala yake wajikite kwenye kilimo cha kutumia zana za kisasa kama matrekta ili kujipatia mazao bora na yenye tija.
Nao washiriki wa maonesho hayo akiwemo mfugaji wa ngo’ombe wa maziwa Lina Joseph Kinabo kutoka kibaha Mkoani Pwani ameelezea ufugaji wa kisasa wa ng’ombe kwa kutumia vifaa vya kisasa kama GPS ambapo hukitumia kutambua maendeleo ya mifugo wake kwa kutumia simu ya mkononi hata anapokuwa mbali na mifugo wake.
Kaulimbiu ya maonesho ya wakulima na wafugaji (nanenane) 2022 ni: Ajenda ya 10/30, Kilimo ni Biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango Bora ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.