Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro wametakiwa kusimamia utendaji kazi wa usafiri wa Pikipiki zilizotolewa na Serikali ya awamu ya sita kwa Waratibu wa Chanjo ngazi ya Wilaya ili pikipiki hizo ziweze kudumu kwa muda mrefu na kufanya kazi iliyokusudiwa .
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima leo Januari 9, 2025 wakati akikabidhi pikipiki 13 kwa Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro, Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi wa Mkoa huo huku akiwataka wakurugenzi kwenda kuzisimamia kwa karibu matumizi yake.
“….namkabidhi DC ambaye ndiye kiongozi Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi wake wakazisimamie zifanye kazi iliyokusudiwa” amesisitiza Kiongozi huyo.
Katika Hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa kutoa pikipiki hizo 13 kwani amesema zitakuwa msaada mkubwa katika suala nzima la uratibu wa Chanjo.
Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi. Prisca Gallet amesema Mkoa umepokea gari moja kwa ajili ya huduma chanjo ngazi ya Mkoa na pikipiki 13 kwa huduma hiyo ngazi ya Wilaya ikiwa ni awamu ya kwanza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba Jamal Idrisa amesema kama halmashauri wanalo gari ya chanjo hata hivyo kutokana na mazingira walikuwa wanapata changamoto namna ya kusambaza chanjo kwa kupatiwa Pikipiki hizo Serikali imesaidia kupunguza changamoto hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ulanga Mhe. Edson William amesema pikipiki hizo zitasaidia waratibu wa chanjo ngazi ya Wilaya kufikisha kwa wakati chanjo hizo kwa akina mama na Watoto hivyo zimeondoa changamoto iliyokuwa imerudisha nyuma zoezi la chanjo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.