Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amewataka Wakuu wa Idara ya Kilimo katika Halmashauri za Mkoa huo Kuimarisha huduma za ugani ili kuwajenge uwezo wakulima kulima mazao yao kisasa.
Agizo hilo amelitoa Mei 10, 2021 wakati wa ufunguzi wa Mafunzo ya wataalam wa kilimo Mkoani Morogoro juu ya utambuzi wa visumbufu vya mazao na namna ya kukabiliana navyo yaliyoendeshwa na Taasisi ya Afya ya Mimea - TPRI katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
‘’…..Hamuwafikii wakulima ipasavyo, mmeitwa wataalam kwa sababu kilimo kinawategemea nyinyi, mkulima anapata utaalam kupitia huduma za ugani, kama hatufanyi maana yake ni nini? nataka ndani ya Mkoa wa Morogoro nyie wataalam muoneshe uwepo wenu’’ amesisitiza Kalobelo.
Mhandisi Kalobelo ameonekana kukasirishwa na kukosekana kwa huduma za ugani kwa wakulima hali ambayo inayopelekea mazao yao kutostawi vizuri kisha kushambuliwa na visumbufu vya mazao bila kuwepo msaada wowote kutoka kwa maafisa hao wenye jukumu la kutoa ujuzi kwa wakulima.
Aidha, Mhandisi Kalobelo amesema hakuna sababu ya msingi ya mazao ya wakulima kushambuliwa na visumbufu vya mazao hivyo kuwataka Wakuu wa Idara ya Kilimo kujiheshisha kupitia Elimu zao kuwaelimisha wakulima namna nzuri ya kulima kwa kisasa na kukabiliana na visumbufu.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Kalobelo amewataka Wakuu hao wa Idara kuwahamasisha wakulima katika maeneo yao kujikita katika kilimo cha pamoja (Block farming) ili kuleta tija ya uzalishaji, kusaidiwa kwa wakati na kupewa taarifa mbalimbali pale majanga yanapojitokeza.
Kwa upande wake Mtaalam wa udhibiti wa visumbufu vya mimea na viwatilifu kutoka TPRI Ndg. Maneno Chidege ametaja leongo la mafunzo hayo ni kutoa Elimu kwa wataalam wa kilimo ili waweze kuwasaidia wakulima kukabiliana na visumbufu wageni ambao wanashambulia mimea katika maeneo yao.
Ndg. Chidege amebainisha baadhi ya visumbufu vya mimea ni Nzige wa Jangwani, panzi, panya, Kantangaze na vijeshi vamizi ambavyo vyote vimeshapatiwa dawa za kukabiliana navyo ikiwa ni pamoja na magonjwa ya mnyauko.
Naye, Kaimu Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Ruth Masengu amesema hali ya visumbufu katika Wilaya hiyo ni tishio hususan visumbufu aina ya kwerea kwerea ambao wanaharibu mazao ya mpunga na vijeshi vamizi wanaoshambulia mazao ya mahindi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.