Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Lyabwene Mutahabwa amewataka walimu wakuu wote Nchini kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia walimu kupata mafunzo endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA).
Dkt. Mutahabwa ametoa agizo hilo Julai 4, 2024 wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wakuu wa shule za Msingi na Sekondari na Maafisa mazingira katika usimamizi wa miradi ya maendeleo yaliyofanyika chuo cha Ualimu cha Morogoro kilichopo Halmashauri ya Manispaa hiyo.
Dkt . Mutahabwa amesema, Serikali imeendelea kuboresha Sekta ya Elimu hivyo mafunzo hayo ya MEWAKA ni muhimu kwa walimu kuyapata yatakayojenga uwezo wa kutoa elimu bora kwa wanafunzi.
"....Nawaelekeza walimu wakuu kote nchini kwenda kuweka mazingira rafiki yatakayowavutia walimu kushiriki kikamilifu mafunzo ya MEWAKA..." Amesisitiza Dkt.Mutahabwa.
Aidha, kiongozi huyo amesema Serikali imekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha elimu msingi ikiwemo kuongezeka kwa uandikishaji wa wanafunzi katika ngazi mbalimbali, kuboreka mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuongezeka kwa wanafunzi wanaomudu stadi za kuandika, kusoma na kuhesabu na kuongezeka kwa ufaulu katika upimaji wa mitiani ya Taifa katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari.
Pia Dkt. Mutahabwa amewataka walimu kuimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji hususan darasa la awali kwa kuwa ndio msingi wa wanafunzi kumudu ( kusoma, kuandika na kuhesabu - KKK ). Uimarishaji huo ametaka uende hata kwenye kuongeza ubunifu katika kutatua changamoto za kujifunza ikiwa ni pamoja na matumizi ya zana na vifaa vilivyo boreshwa katika ufundishaji.
Katika hatua nyingine kiongozi huyo amewasisitiza walimu hao kuweka mifumo ya kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji na ukatili kwa watoto ikiwemo kuundwa kwa vilabu vya wanafunzi ili waweze kujitambua, kujielewa na kujiamini na kushirikiana na jamii katika kubaini masuala ya ukatili na unyanyasaji kwa watoto.
"... Ulinzi na usalama wa mtoto uwe kipaumbele chetu.." amesisitiza kiongozi huyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Program ya BOOST kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Ally Swalehe amesema program hiyo inaimarisha ufanisi wa ujifunzaji na ufundishaji, inaboresha elimu ya awali na msingi pia inatekeleza ujenzi wa miundombinu ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shule 302 zimejengwa nchi nzima ambapo vyumba vya madarasa 7230, matundu ya vyoo 11297 na ukamilishaji wa vyumba vya madarasa 4770 vinaendelea kukamilishwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Elimu Maalum ya watu wazima amesema mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo Maafisa mazingira na wakuu wa shule zinazopokea fedha za ujenzi wa miondombinu kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha usimamizi wa miundombinu na kusimamia manunuzi kwa kuzingatia mfumo wa NEST ili kuondoa changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.