‘Wamachinga’ Morogoro sasa kupatiwa mikopo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amemuagiza Mwenyekiti wa Wafanya biashara ndogo ndogo maarufu kama Wamachinga Mkoani humo Bw. Faustine France kuunda vikundi vya wafanya biashara hao na kuwasilisha maombi ya mikopo yao Ofisi za Halmashauri za Mkoa huo kwa ajili ya kupewa mikopo ya kukuza biashara zao.
Shigela ametoa agizo hilo Oktoba 19 mwaka huu alipokuwa anakagua maeneo yaliyokuwa yanatumiwa na wamachinga yasiyo rasmi kwa ajili ya kufanya biashara zao ili kujiridhisha kama wameondoka na kuhamia kwenye vibanda walivyojengewa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando katika Soko Kuu la Chief Kingalu kwa Kushirikiana na Wahe. Madiwani wa Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (kushoto) akikagua maeneo ambayo yalikuwa yanatumiwa na wamachinga kufanya biashara zao, kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando.
Amesema Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza Halmashauri zote nchini kutenga pesa kwa ajili ya kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu hivyo Mwenyekiti wa machinga aunde vikundi ili wamachinga waweze kunufaika na pesa hiyo kwa kujiunga katika vikundi ili wakopeshwe na kukuza mitaji yao.
‘’….Wamachinga kwa sasa wanajulikana walipo wana namba na anuani, nielekeze Mwenyekiti, unda vikundi peleka kwenye Halmashauri zote, omba kiasi cha fedha unazozihitaji kwa ajili ya vikundi vyako….’’ aliagiza Shigela.
Aidha, amesema mara baada ya Mwenyekiti kuwasilisha maombi ya fedha hizo katika Halmashauri za Mkoa huo atahakikisha anafuatilia mikopo hiyo ili itoke haraka na iweze kuvisaidia vikundi hivyo katika kujikwamua kimaisha.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (wa tatu kushoto) akizungumza na wafanyabiashara ya samaki ambao walikuwa wamebaki katika sehemu ambayo siyo rasmi kufanyia biashara hiyo.
Sambamnba na hayo, Shigela amesema katika maeneno ambayo hayajakamilika rasmi kwa ajili ya kutumika na wamachinga hao, tayari Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro na Mkuu wa Wilaya hiyo wameshakamilisha andiko hivyo wakimkadhi ataliwasilisha TAMISEMI ili watoe fedha kwa ajili ya kukamilisha maeneo ambayo hayajakamilika.
Hata hivyo amewataka baadhi ya wamachinga ambao hawajatoka katika maeneo ambayo yamekatazwa kufanyia biashara kutii sheria bila shuruti kwani muda waliokuwa wamepewa umekwishapita na Serikali imeweka utaratibu huo kwa nia njema ya kuwajengea mfumo mzuri wamachinga kukaa katika maeneo ambayo yameainishwa na kurasimishwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando amempongeza Mkuu wa Mkoa huo kwa ushirikiano wa dhati anaoutoa kwa wamachinga katika kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya biashara zao bila kutumia nguvu katika kutatua changamoto za wamachinga.
Aidha, Msando amesema andiko la kuwasilisha maeneo ambayo hayajakamilika watahakikisha wanalifanyia kazi na kuwasilisha mapema katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili pesa ambazo zimetengwa kwa ajili ya vikundi ziweze kuwanufaisha wamachinga kwa sababu kuna wamachinga vijana, wenye ulemavu na kuna wamachinga kina mama ambao kwa ujumla wana sifa za kupata mkopo huo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (kushoto) akiwa nje ya Soko la Chifu Kingalu akiangalia namna ambavyo atapanua miundombinu ya kufika ndani ya soko hilo.
Naye Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Morogoro Faustine France amewataka wafanyabiashara wote wa mtaa wa Islam, Shani na maeneo mengine ndani ya Manispaa ya Morogoro kutofanya biashara katika maeneo hayo wakisubiria maelekezo ya Serikali ya kuwapeleka maeneo watakayofanyia biashara zao.
Katika hatua nyingine France maarufa kama White amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuunda vikundi hivyo ili kila machinga mwenye uhitaji aweze kupatiwa mkopo kwa ajili ya kukuza biashara yake.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.