Wananchi wa Kijiji cha Wami Luhindo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro wamehamasika kutoa michango yao wa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya msingi ili kuwaokoa watoto wao dhidi ya wanyama wakali na kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 8 kufuata kusoma shule ya Msingi Mawasiliano ambayo iko eneo la Makunganya.
Hayo yamebainika Januari 16 mwaka huu wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare Wilayani mvomero ambapo alifanya mkutano wa hadhara wa kijiji eneo la Wami Vijana maarufu kama Maji chumvi kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Ardhi ambapo baadhi ya wananchi wengi wao inasemekana ni wa kutoka katika Manispaa ya Morogoro ndio waliovamia eneo hilo la wawekezaji na kusababisha mgogoro huo.
Baada ya kuhitimisha changamoto ya mgogoro huo wa ardhi na kuonekana asilimia kubwa ya wakazi wake wameingia kimakosa kwa kurubuniwa na baadhi ya wenyeviti wa Vitongoji katika maeneo hayo ya wawekezaji wanaojulikana kama General Mbowe na Balozi Namfua ndipo wananchi hao wakaibuka na kero ya kutaka kujua ni lini ujenzi wa shule yao utakamilika.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa Kata ya Dakawa Haji Luvanga, ujenzi huo wa shule unaohusisha madarasa manne na Ofisi moja ya mwalimu ulianza mwaka 2013 na haukukamilika kwa wakati kutokana na changamoto ya kujengwa ndani ya eneo la wawekezaji hao.
Hata hivyo Mtendaji Haji Luvanga amesema kwa jitihada za Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Njama Hassan Njama wamefanikiwa kutatua changamoto hiyo na tayari kijiji kimepokea kibali cha kuendelea na ujenzi wa shule hiyo.
Baada ya Taarifa hiyo wananchi walionesha kuahamasika na kumtaka aanzishe mchango kwa ajili ya ujenzi huo na wao wako tayari kuchangia ili shule hiyo iweze kukamilika haraka hivyo kunusuru watoto wao.
Akihitimisha changamoto hiyo ya migogoro ya Ardhi, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewataka wananchi wa kijiji cha Wami Luhindo kufuata sheria katika kupata ardhi huku akiwanyooshea kidole wawekezaji kuwa miongoni mwao ni chanzo cha migogoro ya ardhi Mkoani Morogoro kwa kubaki na maeneo yao kwa muda mrefu bila kuyaendeleza na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.
Kwa sababu hiyo amesema atamwomba Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri wa Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuyafuta umiliki mashamba yote yasiyoendelezwa kwa wakati.
Kuhusu shule, Loata Sanare amesema Elimu ndiyo itawaletea maendeleo wananchi wa Luhindo na hana shaka kijiji hicho watatekeleza kwa ufanisi kwa vile wameonesha shauku katika kujenga shule yao, na kwamba kwa kufanya hivyo siku moja kiongozi mkubwa atatoka katika shule yao.
“ msisubiri mtu mwingine akuleteeni maendeleo, tujitolee…shule hiyo ndiyo itatusaidia, shule hiyo ndio atatoka kiongozi mwingine si dhambi miaka ijayo Mkuu wa Mkoa akatoka mtoto mmoja aliyesoma maji chumvi…” alisema Loata Sanare.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya alimjulisha Mkuu wa Mkoa kuwa siku ya harambee ya kuchangia ujenzi wa shule hiyo itakuwa Januari 20 mwaka huu na kutaka wananchi wote kujitokeza huku akiongelea kuhusu wananchi walioharibiwa mazao yao na wanyama pori na kuhitaji kifuta jasho ambapo jumla ya ekari 11,000 za mashamba ziliharibiwa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.