Jumla ya miche 2140 ya mikarafuu imetolewa kwa wanafunzi 214 wa kidato cha kwanza katika Shule za Sekondari za Mongola na Mgeta Wilayani Mvomero ambapo kila mwanafunzi amepewa miche 10 kwenda kupanda katika maeneo yao ikiwa ni njia ya kupambana na umasikini na kuwasaidia wanafunzi hao kufanikisha ndoto zao za kusoma hadi chuo kikuu.
Miche hiyo imetolewa Mei 13, Mwaka huu na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero inayolenga kuwajengea wanafunzi msingi wa kujitegemea kiuchumi kupitia kilimo cha mikarafuu, zao lenye thamani kubwa kwa sasa katika soko la ndani na kimataifa.
Katibu Tawala huyo amesema Wanafunzi watakaonufaika na sera ya "JISOMESHE NA MKARAFUU" Mkoani humo ni wanafunzi wa kidato cha kwanza wa kila mwaka watapewa miche hiyo ili kuwawezesha wanafunzi hao kujikwamua kiuchumi pamoja na kuweza kulipa ada za shule na chuo watakapofika elimu ya juu hivyo kutokuwa tegemezi kwa wazazi wao ama mikopo.
"Karafuu ina matumizi mengi, na ikitunzwa vizuri, inaweza kuwa msaada mkubwa kwa maisha ya baadaye ya hawa watoto, Tunawalea vijana watakaojitegemea," amesema Dkt. Mussa
Sambamba na hayo, Dkt. Mussa amewaelekeza walimu na jamii kwa ujumla kupanda miche ya zao la mikarafuu katika maeneo ya shule na hata nyumbani, ili kuendeleza utamaduni wa kutumia rasilimali kilimo kama nyenzo ya kukuza elimu na kupambana na umasikini.
Pamoja na ugawaji huo wa miche, wanafunzi wamepatiwa elimu ya msingi kuhusu namna bora ya kuitunza miche hiyo, ikiwemo kuchagua maeneo sahihi ya kupanda, kuitunza kwa maji na mbolea na kujifunza umuhimu wa kuvumilia hadi kipindi cha kuvuna zao hilo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.