Jumla ya Wanafunzi 100 kati ya 650 na walimu 15 kati ya 100 kutoka katika Wilaya tisa za Mkoa wa Morogoro wamefuzu kuendelea na mashindano ya UMITASHUMTA ambapo wataunda timu moja ya kuuwakilisha Mkoa wa Morogoro kitaifa.
Hayo yamebainishwa Juni Mosi, 2021 na Afisa Michezo wa Mkoa wa Morogoro Bi. Grace Njau wakati wa kufunga Michezo ya Umitashumta iliyofanyika katika Shule ya Kilimo ya Kilosa iliyopo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro.
‘’…Ni wanafunzi 100 tu kati ya 650 ambao wamefuzu na walimu karibia 15 tu ambao wataenda kuuwakilisha Mkoa wa Morogoro kitaifa kuanzia Juni 6 hadi 19 mwaka huu Mkoani Mtwara…’’ Ameme Grace.
Aidha, Bi. Grace amesema adhima ya Serikali ya kuandaa mashindano ya Umitashumta kila mwaka ni kuandaa timu itakayo iwakilisha Tanzania katika mashindano ya dunia (World Cup) hivyo Mkoa unapambana kuhakikisha washindi katika mashindano haya wanakuza vipaji vyao na kuviendeleza.
Pia, Bi. Grace amesema Mkoa wa Morogoro ni Miongoni mwa Mikoa bora inayozalisha wanamichezo bora kitaifa na kimataifa hususan kwenye soka la wanaume wakiwemo Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Kibwana Shomari, Hassan Kessy na Kelvin John ambaye anacheza soka la kulipwa nchini Ulaya.
Katika hatua nyingine, Bi. Grace amebainisha changamoto mbalimbali walizokumbana nazo wakati wa mashindano hayo ni baadhi ya walimu kutofundisha michezo kikamilifu mashuleni, ukosefu wa walimu waamuzi wa mpira, ukosefu wa madaktari waliosomea tiba maalumu kwa wachezaji na michango ya Omitashumta kutokamilishwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mgeni rasmi wa mashindano hayo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Ndg. Francis Kaunda, amewataka Walimu waliochaguliwa kuongozana na timu ya Mkoa kuhakikisha wanarudi na ushindi na kuwataka walimu ambao wamekuwa wakipewa timu kisha kurudi bila ushindi wabadilishwe ili kuongeza ushindani.
Sambamba na hayo, Ndg. Kaunda ametoa pongezi kwa wanamichezo walioshinda katika michezo mbalimbali na kuwataka wale ambao hawakufudhu kuunda timu ya Mkoa kuongeza bidii ili mwaka ujao waweze kufanya vizuri Zaidi.
‘’Napenda kuwapongeza wanamichezo wote walioshinda katika michezo mbalimbali na asiyekubali kushindwa si mshindani. Ila kama umeshindwa leo haimaanishi kwamba wewe hujui michezo, unajua ndio maana umefika ngazi ya Mkoa, hivyo uongeze bidii ili mwaka ujao ufanye vizuri’’ Amesema Kaunda.
Mashindano ya Omitashumta Mkoani Morogoro yalianza Mei 30, 2021 baada ya kufunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kilosa ambayo yalihusisha takribani watu 789 wakiwmo walimu na wanamichezo.
Mashindano hayo yalihusisha mpira wa miguu, pete, kengele, nyavu, wavu, mikono, usafi na nidhamu, kwaya na riadha.
Kaulimbiu ya Mashindano hayo ilikuwa ni ‘’ MCHEZO, SANAA KWA MAENDELEO YA VIWANDA’’
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.