WANAFUNZI WALIOFANYA MTIHANI WA MARUDIO WATAKIWA KURIPOTI SHULENI KESHO JANUARI 16,2023.
Wanafunzi waliofanya mtihani wa Marudio wa darasa la saba 2022 na kuchaguliwa kujiunga kidato cha kwanza 2023 wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa kesho Januari 16 Mwaka huu bila kuweka kikwazo chochote ili kwenda pamoja na wanafunzi wenzao kimasomo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe
Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 15 mwaka huu na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Prof. Riziki Shemdoe mbele ya waandishi wa Habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Akifafanua zaidi Prof. Shemdoe amesema wanafunzi hao wamechaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2023 baada ya kurudia mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba uliofanyika tarehe 21 hadi 22 Disemba 2022.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amewaagiza wazazi na walezi wote wa wananfunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika mtihani huo wa marudio kuwapeleka shule watoto wao shuleni bila kuweka kisingizio chochote.
Baadhi ya Viongozi waandamizi ngazi ya Mkoa wakati Katibu Mkuu TAMISEMI akitoa taarifa hiyo. kushoto kwa Katibu Mkuu ni Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa na kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Elimu (Afisa Elimu Mkoa) Bi. Germana Mung'aho
akitoa taarifa hiyo Prof. Shemdoe amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepokea matokeo ya mtihani huo hivi karibuni kutoka Baraza la mitihani la Taifa ambapo jumla ya wanafunzi 2,096 wakiwemo wavulana ni 1,073 na wasichana ni 1,023 sawa na asilimia 96.15 ya watahiniwa waliofanya mtihani wamepata sifa ya kuchaguliwa kujiunga Kidato cha Kwanza katika Shule za Sekondari za Serikali.
Aidha, Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa kushirikiana na Kamati za Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika Mikoa husika imekamilisha zoezi la kuwapangia Shule wanafunzi wote 2,096 katika Shule mbalimbali za Sekondari na Maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hao yamekamilika hivyo wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangiwa.
“Uchaguzi wa Wanafunzi wa Kidato cha Kwanza katika mikoa husika imekamilika zoezi la kuwapangia Shule wanafunzi wote 2,096 katika Shule mbalimbali za Sekondari. Maandalizi ya kuwapokea wanafunzi hao yamekamilika na wanataarifiwa kuripoti katika Shule walizopangiwa siku ya Jumatatu tarehe 16 Januari 2023 ili kuanza masomo.” amesema Prof. Shemdoe.
Sambamba na hilo Prof. Shemdoe ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa wanawaandikisha watoto wao shule za msingi ili waweze kuanza masomo ya awali na darasa la kwanza.
Awali, Baraza la Mitihani la Tanzania lilitoa taarifa ya Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Marudio kwa wanafunzi wa Darasa la Saba mwaka 2022 ambapo jumla ya wanafunzi 2,194 wakiwemo wavulana 1,117 na wasichana 1,077 walitakiwa kufanya mtihani huo kuanzia Disemba 21 – 22, 2022 kwa sababu matokeo yao yalifutwa kwa mujibu wa kifungu 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani 2016 kikisomwa pamoja na kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha sheria cha Baraza la Mitihani Sura ya 107.Jumla ya wanafunzi 2,180 wakiwemo wavulana 1,112 na wasichana 1,068 sawa na asilimia 99.36 walifanya mtihani huo wa marudio.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.