Abel Ngapemba azikwa, viongozi wasifu utendaji kazi wake.
Aliyekuwa Afisa habari Mkuu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza marehemu Abel Ngapemba ambaye alifariki dunia kwa ajali ya gari pamoja na wanahabari wenzake wanne, amepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele Ifakara Wilayani kilombero huku viongozi mbalimbali wakisifu utendaji kazi wake.
Sifa hizo zimetolewa na viongozi wa Serikali na Dini Januari 14, 2022 wakati wa Ibada ya misa takatifu ya kumwombea marehemu Abel iliyoongozwa na Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Ifakara Mhashamu Salutarius Libena katika kanisa Kuu la Mt. Andrea Mjini Ifakara.
Pamoja na Ibada hiyo ya kumuombea marehemu, viongozi wa Serikali kupitia salamu zao za pole, wamesifu maisha ya marehemu Abel Ngapemba namna alivyokuwa anafanya kazi yake na kuishi mbele ya jamii na kutaka wanatasnia wenzake na watu wote kwa jumla kuiga maisha yake.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi alishiriki ibada hiyo takatifu na kutoa salamu za pole kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela.
Katika Salamau zake amewataka watu kila mmoja kwa nafasi yake kuiga mfano wa Abel Ngapemba ambaye aliipenda kazi yake ya utoaji habari kwa wananchi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, kazi aliyoifanya kwa dhati hadi mwisho wa safari yake hapa duniani.
Aidha, Mhe. Hanji Godi godi amewataka watu wote kutoishi kwa usiri katika maisha yao badala yake waishi kwa uwazi zaidi kwa kuwa hatujui siku wala saa kifo kitamfika mtu na cha ghafla kwa kiasi gani kama ilivyotokea kwa Abel.
Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa wote husuan vijana kufanya kazi zao kwa uwazi na wasifanye mambo yao kwa usiri kwa lengo la kutaka kuwa surprise wapendwa wao kwa kuwa vifo kama hivyo vya ghafla vikitokea basi mipango hiyo ya kutaka kuwa surprise wapendwa wao hukosa umaana.
“Kwa sababu kama ukiweka mambo yako kwa usiri ukiondoka unaondoka na vitu vyako vyote na pengine familia yako isinufaike na vitu hivyo ambavyo umetafuta wewe mwenyewe kwa ajili ya familia yako” alisisitiza Mkuu wa Wilaya Hanji Godigodi
Askofu wa Jimbo Katoliki la Ifakara Mhashamu Salutaris Libena ambaye aliongoza misa ya mazishi ya Abel Ngapemba akitoa mahubiri yake kwa waumini walioshiriki misa hiyo iliyofanyika katika kanisa Kuu la Mt. Andrea Ifakara, amewataka watu kumtafuta na kumtafakari Mungu kwa muda wote wa maisha yao yaani kuishi vema wao binafsi na mbele ya jamii inayokuzunguka ili Mwenyezi Mungu atakapomuhitaji akute amejiandaa.
Kwa Upande wake Zamaradi Kawawa kutoka Idara ya Habari Maelezo na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye alitoa salamu kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Serikali, alimwelezea Abel kuwa alikuwa mwanahabari nguli, mwenye weledi wa hali ya juu, katika tasnia hiyo, mzalendo wa kweli, mchapakazi, mnyenyekevu na aliyependa kazi yake. Aidha amesema Abel alikuwa na nidhamu ya kazi ya hali ya juu na akatumia fursa hiyo kuwataka wanatasnia wengine wa habari kuiga mfano wake.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Bi. Nteghenjwa Hoseh akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe, yeye amemwelezea Abel kuwa alikuwa mwanatasnia mwenye uzoefu na alitumika sana katika Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa sababu ya uzoefu wake na kwamba alikuwa kiunganishi kizuri kwa Maafisa habari wanaofanya kazi ndani ya Mkoa wa Mwanza.
Mwakilishi wa ITV na Redio One Mkoa wa Morogoro Idda Mushi amemtaja marehemu Abel kuwa alikuwa na upendo mkubwa kwa mke wake Anna Peter ambaye anafanya kazi Redio One na kuwataka wengine kuiga mfano wa Abel kuishi vema katika ndoa zao kwani amesema upendo wa Abel kwa mkewe ndio uliopelekea mkewe Anna Peter kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa Redio One.
Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. AMINA
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.