WATU 6000 WILAYANI VIJIJI VYA IYOGWE NA KINYOLISI WILAYANI GAIRO KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI
Wananchi zaidi ya 6000 wa kijiji cha Iyogwe Wilayani Gairo Mkoani Morogoro wako mbioni kupata maji safi na Salama baada ya Serikali ya awamu ya sita kupeleka zaidi ya Tsh. 500Mil. Kwa ajili ya kuwaondolea wananchi wa kijiji hicho kero hiyo ya Maji.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya siku mbili ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Wilayani humo ambapo pamoja na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, ametembelea mradi wa Maji wa utakaogharimu Tsh. 513Mil. Ambapo utanufaisha wananchi 6000 wa vijiji viwili vya Iyogwe na Kinyolisi.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kinyolisi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (hayupo pichani) alipofanya ziara kijijini hapo Mei, 25 mwaka huu
Akiwa katika kijiji cha Kinyolisi ambapo mradi huo unatekelezwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela pamoja na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazanaia amemuagiza Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wa Wilaya ya Gairo Paascal Jeremia kuhakikisha mradi huo unakamilika mwezi juni mwaka huu ili kuwaondolea wananchi kero ya maji waliyokuwa wanaipata.
“Meneja wa RUWASA nikuagize nataka tarehe therathini uje ujaribu vituo vyote kama vinatoa maji kwenye kituo hiki ili wananchi wetu wanaohangaika kupata maji waweze kupata maji” amesema Shigela.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza wananchi wa Kata ya Iyogwe kujitokeza kwa wingi wakati wa zoezi la Sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 Mwaka huu ili serikali kupata takwimu sahihi zitakazosaidia utoaji wa huduma mbalimbali za Maendeleo ya wananchi kwa uhakika zaidi.
Mkuu wa Wilaya ya Gairo Omary Makame akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuongea na wananchi wa Kijiji cha Iyogwe alipofanya ziaya Wilayani humo
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Gairo Jabiri Omary Makame amebainisha kuwa kukamilika kwa mradi wa maji wa Kinyolisi kutawasaidia wananchi wa eneo kujihusisha na masuala ya maendeleo zaidi badala ya kutafuta maji kwani kwa sasa wananchi hao wanatumia maji ya visima tena kwa hupanga foleni hivyo kupoteza muda mwingi.
Mhe. Recho Nyangasi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wialya ya Gairo wakati wa mkutano wa hadhara Kijiji cha Iyogwe wakati ziara ya Mkuu wa Mkoa
Naye diwani wa kata ya Chakwale Mhe. Ramadhani Kimwaga pamoja na kuishukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo, ameeleza changamoto zinazoikabili Kata hiyo kuwa ni pamoja na changamoto ya miundombinu ya barabara yakiwemo madaraja.
Kwa upande wake Steven Mchongi ambaye ni mwenyekiti wa Shule ya msingi Kilimani amemuomba Mkuu wa Mkoa kutatua changamoto ya madawati inayoikabilia shule yake ambayo wanafunzi zaidi ya 304 hawana madawati ya kukalia.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.