Wananchi wa Kata ya Dumila Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wameiomba Serikali kuwachukulia hatua viongozi waliohusika na upotevu wa pesa zaidi ya Shilingi Mil. 800 zilizotolewa na Benki ya Dunia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji.
Wananchi wametoa ombi hilo Oktoba 5 mwaka huu mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela alipofanya ziara ya siku moja Wilayani Kilosa kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo, kusikiliza na kutatua kero za wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Wananchi wa kata ya Dumila wakiwa katika mkutano wa hadhara wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akitoa maelekezo juu ya kero zao.
Akizungumza katika Mkutano huo mwananchi Issa Mkumbuko amesema Novemba 2011 Serikali ilipeleka shilingi Mil. 800 zilizofadhiliwa na Benki ya dunia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji katika kata ya Dumila lakini pesa hizo hazikutumika kufanya miundombinu hiyo.
‘’….Milioni 800 zilizotolewa na World Bank zimepotea kama ice cream motoni hazijulikani zilipo, hizo milioni zimepotea hazijafanya kazi hadi sasa’’…. amesema Mkumbuko.
Katika hatua nyingine mwananchi huyo amesema mbali na Serikali kutoa pesa hizo tayari wananchi walikuwa wamechanga jumla ya shilingi Mil. 18 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo ambazo nazo hazijulikani matumizi yake.
Mmoja kati ya wananchi waliohudhuria mkutano huo akitoa kero kwa niaba ya wananchi wa kata ya Dumila.
Naye Joseph Kosmas amebainisha changamoto nyingine inayowakabili wananchi wa Dumila kuhusu changamoto ya maji ni kutokuwepo kwa chombo cha kutoa huduma ya maji ambacho kingesaidia kutatua kero za maji na kurahisisha upatikanaji wa maji katika kata hiyo.
Amesema Uongozi wa uliopo wa chombo hicho imeundwa na watu kwa wachache kwa maslahi yao binafsi na hakijishughulishi na lolote katika kutengeneza miundombinu ya maji lakini pia jumuiya hiyo inajiendesha yenyewe bila wataalam wala mwakilishi kutoka kwa wananchi.
Baada ya kutolewa kero hizo za wananchi Mkuu wa Mkoa Martine Shigela amefikia uamuzi wa kuvunja Uongozi wa chombo hicho cha kutoa huduma ya maji kilichokuwepo na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga kwa kushirikiana na Mhandisi wa maji kutoka RUWASA Wilaya hiyo Joshi Chum kuitisha mkutano kwa ajili ya kuunda jumuiya mpya ya maji ambayo itaundwa kwa mujibu wa sheria na sifa zinazotambulika kwa lengo la kusimamia miundombinu ya maji.
Aidha, Shigela amesema mara baada ya kuundwa kwa chombo hicho lazima kiwajibika kwa wananchi kwa kuwafikishia huduma ya maji hususan katika vijiji ambavyo hadi sasa vinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji.
Katika hatua nyingine Shigela amesema kutokana na uhitaji mkubwa wa maji katika Kata ya Dumila bado ameelekeza visima vya maji vinavyomilikiwa na Bw. Ndunda kuendelea kutoa huduma ya maji kwa wananchi bila kuzuiwa na mtu yoyote.
‘’Kwa hiyo Bw. Ndunda kama una pesa yako umehifadhi benki Milioni 200 kazichukue nenda sehemu yoyote ambayo unadhani wananchi wanahitaji maji wapelekee’’ ameagiza Shigela.
Akijibu tuhuma za upotevu wa fedha zinazodaiwa kupotea na kutumika ovyo ambazo zilitolewa na World Bank kupitia Serikali ya Tanznaia na zile zilizochangwa na wananchi, Mhandisi wa maji Wilaya ya Kilosa Joshi Chum amekiri kuletwa fedha hizo na kwamba zilitumika katika ujenzi wa miundombinu iliyopo kwa sasa ikiwa ni pamoja na kujenga visima viwili.
Aidha fedha hizo zilijenga tenki la maji la lita 300,000, zilinunua mambomba yaliyolazwa umbali wa Km 28, kujenga vituo 56 vya maji, kununua pampu ya umeme na kujenga nyumba ya kuhifadhia pampu hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga akizungumza na wananchi wa kata ya Dumila.
Kuhusu fedha zilizochangwa na wananchi Mhandisi Chum amesema anachokijua ni shilingi Mil. 9 zilitumika kununulia mita ya Umeme huku nyingine zikitumika kwa ajili ya uendeshaji wa chombo hicho kutoa huduma ya maji huku akisema kiasi kingine inaonesha kweli matumizi yake hayakuwa kwenye utatratibu na suala hilo linafanyiwa kazi ili kuwachukulia hatua za kisheria watakaobainika kuhusika nazo.
Pamoja na majibu hayo, Mhandisi Chum amekiri kupokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa na kwamba anaendelea kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuratibu upya uundwaji wa chombo cha kutoa huduma ya maji katika kata ya Dumila.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa ametembelea Kata tatu za Mtumbatu na Dumila ambako alifanya mikutano ya hadhara na kutatua kero za wananchi pamoja na kukagua ujenzi wa daraja la Kiegea ambalo hadi sasa limefikia asilimia 90 ya ujenzi wake.
MWISHO
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.