Wananchi wa Kijiji cha Chanzuru wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wameipongeza serikali kwa kuingilia kati mgogoro wa shamba lenye jumla ya Ekari 1598 uliokuwepo baina yao na mwekezaji Mihanga Leizer ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 15 bila kutatuliwa.
Hatua ya kuipongeza Serikali inakuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela kufika Kijijini hapo Julai 26 mwaka huu na kueleza msimamo wa Serikali juu ya mgogoro wa shamba hilo kutoka kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shigela amesema, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo kuwa shamba hilo lirudishwe kwa wananchi kwa ajili ya kulitumia kufanya shughuli zao za kuwaletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kilimo.
Kutokana na maelekezo hayo, Mkuu wa Mkoa huyo amempiga marufuku Mwekezaji Leizer kufanya shuguli yoyote ya kilimo ikiwa ni pamoja na kutovuna mazao ya wananchi aliyoyakuta huku akimtaka kutii maelekezo aliyopewa ili kuepusha usumbufu unaoweza kujitokeza.
‘’Ukitaka kuchukua ardhi na ukakuta kuna maendelezo ambayo yamefanyika ni lazima kulipa fidia kwa maendeleo yaliyofanyika, hivyo kuanzia leo ni marufuku kwa ndugu Laizer kuvuna mazao ambayo aliyakuta kwenye shamba hilo’’amesema Shigela.
Licha ya kumpiga marufuku mwekezaji huyo kuvuna mazao ya wananchi aliyakuta katika shamba hilo, Shigela amemruhusu kuvuna mazao ambayo alipanda mwenyewe katika shamba hilo huku Serikali ikitafuta namna nzuri ya kutatua mgogoro huo.
Sambamba na hayo, Shigela amesema Serikali itatambua pesa ambazo Mwekezaji huyo amezitumia katika shamba hilo lakini pia Serikali itatatambua na kuthamini wananchi zaidi ya 4000 waliopo katika kata ya Chanzulu wanaotumia hekari zaidi ya 1200 kwenye shamba hilo lenye hekari 1500
Kwa upande wake Kamishina wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Morogoro Frank Mizikuntwe amesema shamba hilo lilifutwa mwaka 2017 na mwaka 2018 likafanyiwa mpango wa matumizi bora ya Ardhi.
Aidha, Mizikuntwe amesema kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alielekeza sehemu ya shamba hilo ambayo haifanyiwi matumizi yoyote ya kibinadamu apewe mwekezaji huyo na sehemu ambayo wananchi wanatumia kwa makazi, mazao ya muda mrefu na muda mfupi wananchi hao waiendeleze kwa shughuli hizo.
Kwa upande wake mwekezaji Mihanga Laizer, amesema shamba hilo alilinunua kwa shilingi Mil. 90 na kukabidhiwa nyaraka zote za msingi kwa kufuata sheria zote za ununuzi wa ardhi zilizoendeshwa na wanasheria wa mahakama ya Wilaya ya Kilosa Mkoani humo.
Mihanga amesema baada ya kununua shamba hilo aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kilosa kuomba kuainishiwa mipaka ya shamba hilo ambapo wataalam kutoka Wilayani Kilosa walifika shambani hapo na kumuwekea mipaka kwenye shamba lake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji hicho cha chanzulu akiwemo Shabani Shomvi wamempongeza Mkuu wa Mkoa Martine Shigela kwa kutatua Mgogoro huo uliodumu kwa kipindi kirefu na kumuomba afike katika vijiji vingine kutatua migogoro hiyo ya Ardhi kikiwemo kijiji cha Ilonga.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.