Mhandisi Mahundi awataka wananchi Malinyi kuchangia maji.
Naibu Waziri, Wizara ya maji Mhandisi MarryPrisca Mahundi amewataka wananchi Wilayani Malinyi kuendelea kuchangia gharama ndogo za maji zinazotozwa na mamlaka husika ili kuendelea kupata huduma ya maji safi na salama.
Naibu Waziri amesema hayo Januari 17 mwaka huu wakati wa ziara yake Mkoani Morogoro na kukutana na wananchi wa Wilaya hiyo ambapo alitembelea miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa katika Wilaya hiyo kupitia Wakala wa Usambazaji wa Maji safi na Usafi wa Mazingira-RUWASA.
Naibu Waziri amesema kuwa miradi hiyo inatekelezwa kupitia fedha za UVIKO 19 ambapo Wilaya ya Malinyi imepokea kiasi cha shilingi milioni 641 zilizotolewa na Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan, fedha hizo zitasaidia kutekeleza mradi mkubwa wa maji ambao utapeleka maji katika Kata za Changani, Itete njiwa pamoja na uchimbaji wa visima 14 mradi ambao utatekelezwa na wakandarasi watano.
“………. sisi tunaotumia tunachangishwa hatuuziwi maji, uongo? ninawasihi kuendelea kuchangia gharama ndogo za maji ambazo mnapangiana kulingana na mazingira yenu…….” alisisitiza Waziri.
Aidha, Mhandisi Mahundi amesema kuwa lengo la Wizara sio kuwauzia maji wananchi wake isipokuwa wananchi wanapaswa kuchangia gharama za uendeshaji wa miradi ya maji kupitia michango hiyo wanayochangishwa ili kununulia madawa ya kutibu maji Pamoja na kununua umeme utakaotumika kusukuma hayo maji.
Sambamba na hilo Naibu Waziri amefafanua kuwa mradi huo wa uchimbaji wa visima 14 vya maji utatoa ajira kwa wakazi wa Wilaya hiyo pamoja na kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa eneo la mradi hivyo wananchi waendelee kutunza miundo mbinu ya maji.
Akitoa shukrani zake kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Jimbo la Mlinyi Antipass Mgungusi amesifu kasi hiyo ya utendaji kazi wa Rais Samia na Serikali yake ya awamu ya sita ya kuhakikisha kuwa wananchi wake wanaondokana na changamoto ya maji na changamoto zingine kama vile umeme barabara na kwamba kupitia kasi hiyo mradi huo wa maji anaamini utakamilika kabla ya awamu ya pili ya uongozi wa Rais Samia.
Kwa upande wao wananchi wa Kitongoji cha Makugila A, katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Bi. Asha kwa niaba ya wananchi wenzake ameeleza adha waliyokuwa wanaipata na kwamba kutokana na ukame, ulipelekea wao kutumia maji machafu yenye tope hali ambayo ilipelekea kuugua homa ya matumbo Pamoja na kuhara.
Hata hivyo wananchi hao wanaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kuwasogezea huduma za maji safi na salama katika maeneo yao.
Wilaya ya Malinyi inavituo 643 vinavyotoa huduma ya Maji Kati ya 703 vilivyopo. Takribani fedha Bilioni 3 Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 zimetengwa Kwa ajili ya kutatua changamoto ya Maji katika Wilaya hiyo.
Kwa sasa Hali ya upatikanaji wa Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi umefikia asilimia 70 ambapo zaidi ya wakazi 1400 wanapata huduma hiyo huku asilimia hiyo ikiwa nyuma ya lengo la Serikali kupitia Wizara ya Maji ya kuhakikisha kuwa upatikanaji wa Maji unafikia asilimia 85 vijijini na 95 mjini.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.