Wananchi Mkoani Morogoro watakiwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO 19 katika vituo vyote vya afya vinavyotoa huduma ya chanjo ili wawe salama na kuwakinga wengine dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Wito huo umetolewa Novemba 19 mwaka huu na Dkt. Florian Tinuga Meneja wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya wakati wa uzinduzi wa Awamu ya pili ya chanjo ya UVIKO -19 Mkoani Morogoro uliofanyika katika viwanja vya Jamhuri, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Dkt. Florian Tinuga amesema Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa na mwitikio hafifu wa chanjo hiyo ambapo kwa sasa wananchi walio chanja ni asilimia 66.2 ukilinganisha na lengo la Taifa la asilimia 80.
Wahudumu wa Afya ambao wameandaliwa kutoa huduma ya chanjo ya Uviko - 19 kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Dkt. Florian Tinuga amesema ili Mkoa huo ufikie lengo hilo ifikapo Disemba mwaka huu uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wananchi unatakiwa kuendelea katika maeneo yote ndani ya mkoa Pamoja na kusogeza huduma hiyo ya chanjo karibu na wananchi.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua taadhari ya ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya kwa kuwa ugonjwa bado ni tishio uliwenguni.
Meneja wa Mpango wa chanjo Taifa Dkt. Florian Tinuga (kushoto), Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa (katikati), na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio pamoja na Mwakilishi wa Wizara ya Afya wakishuhudia uzinduzi wa chanjo katika Mkoa huo.
Sambamba na hilo, Gerson Msigwa amewataka watanzania kuchukua taadhari ya ugonjwa wa Ebola ambao upo katika nchi Jirani za Uganda na Kongo, pia amewataka kutoa taarifa kwa wataalamu wa Afya pindi wanapoona viashiria vya ugonjwa wa Ebola.
Aidha, Gerson Msigwa amesema Serikali imechukua taadhari kwenye mipaka yote ya nchi na katika viwanja vya ndege vinavyopokea wageni kutoka nje ya nchi ili kubaini watu wenye viashiria vya ugonjwa huo tishio kwa sasa.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa ameishukuru Wizara ya Afya kwa kuzindua mpango wa chanjo ya Uviko 19 katika mkoa huo na kusema kuwa wananchi wapo tayari kwa zoezi la uchanjaji.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando akihamasisha wananchi kupata chanjo ya Uviko - 19 katika Mkoa huo.
Aidha, Mhe. Albert Msando amewahakikishia wakazi wa mkoa huo kuwa chanjo hizo ni salama na hazina madhara yoyote kwa afya zao na kuwataka kupuuzia maneno ya upotoshaji yanayozushwa na baadhi ya watu wasio na mapenzi mema na nchi yetu au wasio na uelewa wa kitaalam juu ya chanjo hizo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kuhakikisha zinatoa elimu kwa wananchi wake ili wahamasike kuchanja Pamoja na kuwasogezea huduma hizo za chanjo karibu maeneo wanayoishi.
Wananchi wa Mkoa wa Morogoro wakishuhudia uzinduzi wa chanjo ya Uviko - 19 katika Mkoa huo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.