Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amewataka wananchi Mkoani humo hususan kwa kaya zitakazofikiwa na Wadadisi au watafiti wa zoezi hilo kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha tafiti hizo za kitafiti.
Mhe. Malima ametoa wito huo Disemba 20, 2023 wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari uliofanyika ofisini kwake ukiwa na lengo la kuhamasisha wananchi mkoani humo kushiriki zoezi la kitaifa tafiti za kitakwimu.
Amesema, tafiti hizo zitaisaidia Serikali katika ugawaji wa Rasilimali za Taifa, kuongeza wigo wa utoaji wa huduma za jamii, ujenzi wa miundombinu na miradi mingine ya maendeleo, hivyo, amewataka wananchi kushiriki na kutoa takwimu sahihi kwa wadadisi hususan wale watakaofikiwa kwan huo ndio utakuwz mchango wao katika kufanikisha zoezi hilo la kitaifa.
“...kushiriki tafiti kama hizi ni sehemu ya mchango wako mwananchi katika kuleta maendeleo ya Mkoa wetu na ya nchi nzima...shime wananchi tushirikiane kuyatekeleza haya...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, amezitaja tafiti hizo ambazo tayari zimeanza Novemba 2023, kuwa ni pamoja na Utafiti wa Shughuli za Kiuchumi na Kijamii ukilenga kupata idadi ya shughuli za kiuchumi na kijamii zilizopo katika sekta rasmi na Utafiti wa Kilimo wa mwaka 2022/2023 ambao lengo lake ni kufuatilia maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Malima amesema utafiti wa Kilimo ni muhimu kwa Mkoa huo kwani Mkoa huo umedhamiria kuwa mfano katika mapinduzi ya Sekta ya Kilimo hapa nchini kutokana na Mkoa huo kujikita katika kilimo biashara kupitia mazao mkakati matano ya Michikichi, Parachichi, Karafuu, Kakao na Kahawa ambapo wanatarajia kuzalisha miche milioni moja kwa kila zao.
Hivyo, Mkuu wa Mkoa Adam Malima amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoani Morogoro na Viongozi wengine wa ngazi ya Kata, Vitongoji na Mitaa kuwa seheme ya kufanikisha zoezi la tafiti hizo kwa kuhakikisha wananchi wao kutoa ushirikano utakaohitajika kwa Wadadisi watakao husika na ukusanyaji wa takwimu hizo.
Kwa upande wake Meneja Takwimu Mkoa wa Morogoro Bw. Charles Mtabo amesema kuwa tafiti hizo ni miongoni mwa tafiti ambazo hufanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na zitafanyika kwa kipindi cha miezi miwili ambapo kwa Mkoa wa Morogoro tafiti hizo zitafanyika katika maeneo 66.
Utafiti wa Kilimo wa Mwaka 2022/23 unafanyika katika jumla ya maeneo 1352 kati ya maeneo hayo 1234 ni Tanzania Bara na maeneo 118 ni ya Zanzibar. Jumla ya Kaya 16224 zinatarajiwa kufanyiwa mahojiano na wadadisi au watafiti walioaminiwa na serikali.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.