Wananchi Mkoani Morogoro wameiomba Serikali kusogeza huduma ya wataalamu wa sheria karibu yao ili kuwasaidia katika kuwafikia na kupata ushauri wa kisheria kwa kuwa wanasheria hao kwa sasa wako nao na kunapelekea wananchi walio wengi kushindwa kuwafikia na kupata msaada wa kisheria kwa sababu ya gharama kubwa inayosababishwa na umbali kutoka maeneo walipo.
Wananchi hao wametoa Ombi hilo hivi karibuni walipohojiwa na kituo hiki na kutoa maoni hayo wakati wa kikao cha siku tatu cha Wanasheria wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Morogoro kilichofanyika katika Mji mdogo wa Dumila Wilayani Kilosa Mkoani humo.
Wananchi hao waliotoa maoni hayo kwa nyakati tofauti, Faustini Andrea wa Dumila Wilayani Kilosa aliomba Serikali kusogeza wataalamu hao wa sheria katika ngazi za chini kwa kuwa mwananchi wa kawaida ni vigumu kumudu gharama ya kumfuata mwanasheria katika Ofisi za Halmashauri, hivyo aliiomba Serikali kusogeza Ofisi za wanasheria hao karibu na wananchi ili wanapohitaji msaada wa kisheria iwe rahisi kuwafikia.
“wanasheria wapo Wilayani ila wanakaa mbali sana na Jamii. kwa huku kijijini kumpata mwanasheria kuja kumsaidia mwananchi mmoja ni ngumu na mwananchi kutoka hapa kwenda Wilayani kwenda kumtafuta mwanasheria anakuwa hajui process aanzie wapi amalizie wapi, kwa hiyo tunaomba Serikali kusogeza wanasheria karibu au kufungua Branchi au Ofisi kwa kila kijiji kwa ajili ya huduma ya wananchi” alisema Faustini Andrea.
Naye Mwanahamisi Ayubu wa kijiji cha Magole Wilayani Kilosa alisema anajua kuwa wapo wanasheria wa Serikali ngazi ya Wilaya na kwamba wanasaidia kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi, shida ipo kwa wananchi wengi kutojua uwepo wa wanasheria wa Halmashauri na kwamba wananchi wanaweza kuwatumia katika kuwaomba msaada wa kisheria, hivyo ameiomba Serikali kufikisha Elimu hiyo kwa wananchi namna ya kuwafikia wanasheria hao.
Naibu Mkurugenzi wa Sheria kutoka TAMISEMI Idara ya Mashitaka, Eustard Ngatale akiongea mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo alikumbusha majukumu ya wanasheria wa Serikali za mitaa na kwamba bila wanatasinia hao wa Sheria hao, Halmashauri za Serikali za Mitaa haziwezi kufanya kazi zao kikamilifu na kwa mafanikio yanayotegemewa.
Ngatale amesema Wanasheria wa Halmashauri wapo pale kwa ajili ya kuhakikisha shughuli zote za Kiserikali zinafanyika ndani ya Halmashauri husika na zinafanyika kwa mujibu wa Sheria za Tanzania na kwamba kila Mkurugenzi katika Halmashauri yake kila jambo analofanya lazima azingatie sheria, hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri hawezi kufanya kazi zake kwa ufanisi endapo mwanasheria atakosekana katika Halmashauri yake.
“Mkurugenzi yeyote aliye ‘smart’ anayefanya vizuri, kabla ya maamuzi hajafanya lazima apate ushauri kutoka kwa mwanasheria” alisema Ngatare na kusisitiza kuwa ni katika misingi hiyo halmashauri zitafanya kazi zao kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Katiba .
Katika Hatua nyingine Naibu Mkurunenzi huyo wa Sheria alimpongeza Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo kwanza kwa kuthamini tasnia ya wanasheria kwamba huwezi kufanya kazi bila wanasheria, lakini pia kwa ubunifu wake wa kuwaunganisha wanasheria ndani ya Mkoa na kufanya vikao nao kwa lengo la kubadilishana uzoefu lakini pia kuwabana na kuwapima kupitia taarifa mbalimbali za kesi kwa lengo lakuhuisha utendaji kazi wao na hivyo kuwa msaada zaidi kwa watanzania.
Akifungua kikao hicho cha Wanasheria wa Serikali za Mitaa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo, amewataka wanasheria wote wa Serikali za Mitaa kuwa sehemu ya kuandaa mikataba mbalimbali ya miradi ya maendeleo ili serikali iwe salama katika kutekeleza miradi husika na kunapotokea migogoro katika mkataba huo Serikali isipate hasara kwa sababu ya mkataba kuandaliwa vibaya ama mwanasheria kukosa kushirikishwa kwenye uandaaji wa mikataba hiyo.
Sambamba na agizo hilo amewataka pia wanasheria kuhakikisha wanarekebisha au kuhuisha sheria ndogo ili ziweze kutekelezeka kulingana na wakati uliopo na haziingiliani na sheria mama au sheria ndogo nyingine. Aidha, ametoa miezi miwili kwa wanasheria hao Mkoani humo kuwasilisha katika Ofisi yake taarifa inayoonesha sheria ndogo zinazotakiwa kufanyiwa marekebisho ambazo zinaonekana zimepitwa na wakati na au hazitekelezeki.
Nao wanasheria wa Serikali za Mitaa wakiwakilishwa na Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Elikarim Tea, wametaja changamoto kubwa wanayokumbana nayo kuwa ni wananchi kukimbilia ngazi za juu wanapokuwa na kesi badala ya kufuata ngazi husika wakiamini kuwa watasaidiwa mapema shida changamoto zao kutoa wito kwao mara wanapohitaji misaada ya kisheria ni vema kuonana na wanasheria katika halmashauri zao ili wasaidiwe mapema kuliko kukimbilia ngazi za juu na matokeo yake kutopata msaada wanaohitaji mapema au madai yao yanapelekea kuchelewa kutatuliwa kwa kuwa yanakuwa yamepitia katika milolongo mirefu pasipo sababu za msingi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.