Wananchi wa Kijiji cha Chanzuru Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamefurahishwa na uamuzi wa Serikali uliotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim majaliwa (MB) wa kufuta shamba la Mwekezaji Laizer Mihanga na kugiza shamba hilo kupewa wananchi wa Kijiji hicho kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Taarifa ya kufutwa shamba hilo lenye Ekari 1598 uliwasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela Septemba 8, mwaka huu alipofanya ziara Wilayani Kilosa kwa lengo la kuwasilisha uamuzi huo wa Serikali uliotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.
Shigela amesema amefanya ziara hiyo Wilayani humo kutekeleza agizo la Waziri Mkuu kufuta shamba hilo la Mkonge la Chanzuru ambalo awali lilikuwa linamilikiwa na Mwekezaji Mzawa Laizer Mihanga na kwamba kwa sasa Serikali imeamua shamba hilo wapewe wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Shigela amesema maelekezo ya Mhe. Majaliwa yanaelekeza Hekari 1200 kati 1598 zitarejeshwa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli hizo za maendeleo na Hekari 398 zitabaki kwa Mwekezaji Laizer Mihanga ambaye alikuwa anamiliki shamba hilo hapo awali.
‘’…Sasa Serikali imechukua hatua zifuatazo, kwanza lile shamba limefutwa ni mali ya Serikali, kwa hiyo hakuna mwenye kusema ana shamba lake…’’ amesema Shigela.
Aidha, Shigela amefuta kesi zilizokuwepo baina ya Mihanga na wananchi zinazohusu shamba la Chanzuru, amepiga marufuku mwananchi yoyote kukamatwa ama kuondolewa wakati anafanya shuguli zake za kimaendeleo alizokuwa anazifanya ndani ya shamba hilo na kuwataka wananchi hao kuwa huru kuendelea na majukumu yao bila kubugudhiwa.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema baada ya shamba hilo kuchukuliwa na Serikali na kulitoa kwa wananchi kazi inayofuata ni kuweka utaratibu wa namna ya kuligawa kwa wananchi hao ili kuweka usawa katika kugawana badala kila mmoja kujitwalia eneo kwa ukubwa anaoutaka hali itakayoleta tena migogoro kwao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Majid Mwanga amekiri kupokea maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo hayo ya Waziri Mkuu na kumuhakikishia kudumisha ulinzi, Amani na usalama kwa wananchi wa Chanzuru na pamoja na mali zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wa Kijiji cha Chanzuru wameonesha furaha yao juu ya uamuzi wa Serikali wa kufuta shamba hilo akiwemo Ally Omary, huku wakimuomba Mkuu wa Mkoa kuunda kamati kwa ajili ya kuweka mipaka ya eneo lote la Ekari 1,200 walilopewa ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza tena.
Naye, Mkude Omary, licha ya furaha na pongezi kwa Mkuu wa Mkoa, amemuomba Hekari 368 zilizobaki kwa ajili ya Mwekezaji Laizer zirudishwe kwa wananchi kwa sababu Mwekezaji huyo alikuta Mikonge katika shamba hilo ambayo ilikuwa linalimwa na wananchi wa kijiji hicho.
Mwekezaji Laizer Mihanga ambaye muda mwingi amekuwa akidai kuwa shamba la Mikonge la chanzuru lenye ukubwa wa Ekari 1,598 ni mali yake kwa sasa amepewa jumla ya Ekari 398 kwa ajili ya kuendelea na shughuli za kilimo cha zao hilo la Mkonge alichokuwa akikiendesha.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.