Wananchi wa Kijiji cha Mabula Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wameaswa kutunza na kulinda mradi wa maji uliofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision ili kuuwezesha mradi huo kudumu kwa muda mrefu na kuwaletea maendeleo yao.
Ushauri huo kwa wananchi wa Kijiji hicho umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare Novemba 25 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Mradi huo baada ya kukamilika na kuwapunguzia wanawake mzigo wa kutafuta maji umbali mrefu.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema ili mradi huo uwe endelevu ni lazima Kamati ya watumia maji iundwe na hiyo ndiyo itaratibu namna nzuri ya kuuendeleza mradi na itaratibu pia namna ya kuutunza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kisima cha maji kwa ajili ya mradi huo kinazungushiwa uzio.
“haya maji tusipoyapangilia vizuri kuna siku yatakatika, na kamati ile iratibu namna ya kupata koki mara itakapokuwa imeharibika… Sasa namna ya kufanya ni kuandaa kamati ya maji ya kijiji chini ya viongozi tuliowachagua” alisema Sanare.
Pamoja na ushauri alioutoa juu ya kuunda Kamati kwa ajili ya kusimamia mradi na kuufanya kuwa endelevu kwa kuwapa elimu wananchi kuchanga fedha kidogo itakayoendeleza mradi, Loata Sanare amewaonya viongozi wa Kijiji kutoingilia majukumu ya kamati itakayoundwa na kufuja fedha za mradi huo zitakazochangwa na wananchi kwani wakibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi kutoka Word Vision Bw. Donasian Severine amesema lengo la Mradi wa maji katika Kijiji cha Mabula ni kushirikiana na jamii na wadau wengine kuhakikisha maisha ya mtoto yanastawi katika Nyanja zote za elimu, Afya na Ulinzi na Usalama. Huku akibainisha kuwa mradi huo utanufaisha wakazi 3,322 wa vijjij wa kijiji cha mabula.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ameishukuru shirika lisilo la kiserikali la Word Vision kwa uhisani wanaoutoa katika Wilaya ya Kilosa katika kutatua kero za wananchi na kuwaletea maendeleo yao kwenye sekta za Elimu, Afya na sekta nyingine ndani ya Wilaya hiyo hususan katika Tarafa za Magole na Ulaya.
Naye mwakilishi wa RUWASA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joshi Chumu amesema mradi huo umetekelezwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi 220 Mil. huku akiahidi kutoa Elimu kwa wananchi namna ya kuunda jumuiya kwa lengo la kuendeleza Mradi huo.
Mradi huo unaofadhiliwa na World Vision unatekelezwa katika Kata sita na vijiji 21 ndani ya Wilaya ya Kilosa Mkoani humo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.