Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro wamemuomba Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela kutatua kero mbalimbali wanazokumbana nazo ili kurahisisha shughuli za maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Wananchi wametoa maombi hayo June 12, mwaka huu katika Mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza kero wanazokumbana nazo na kuzitolea maamuzi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao akiwemo Ndg. Hassan Issa, amesema wanakabiliwa na miundombinu mibovu ya barabara ya Malinyi – Ifakara hali inayopelekea kushindwa kusafirisha bidhaa zao kutokana naubovu wa miundombinu hiyo hususan kipindi cha masika.
Aidha, Ndg. Issa ameiomba Serikali iwatengenezee barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili waweze kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi, hivyo kukuza uchumi wao, Mkoa na taifa kwa jumla.
‘’…..Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kwa muda mrefu sasa tuna changamoto ya barabara, wakandarasi ambao walipewa barabara hii huonekana pale tu mvua zinapoanza kunyesha, nyakati za kiangazi hawashughuliki na barabara hii, kiukweli tunateseka sana,.’’ amesema Ndg. Issa.
Sambamba na hayo, ametoa ombi kwa Mkuu huyo wa Mkoa kuwakamilishia vituo vya Afya ili kuwasogezea huduma karibu wananchi ambao wanatembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.
Naye Anitha Bondwa, amebainisha kero ya wauguzi ambao wanawachangisha fedha kwa ajili ya matibabu licha ya kuwa na bima za Afya ambazo kwa mujibu wa maelezo yake haziwasaidii pindi wanapohitaji huduma za matibabu katika vituo vya Afya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Masele amesema hadi sasa wamefanikiwa kupata zaidi ya shilingi Milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Malinyi, Bilo na zahanati ya Madabadaba ambazo zikikamilia zitasaidia kuondoa changamoto ya umbali mrefu wa kufuata huduma za Afya.
Akizungumza na wananchi wa Malinyi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela, ametoa maelekezo mbalimbali na kutatua changamoto za wananchi hao ambapo amemtaka Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo kufuta utaratibu wa wagonjwa kulipa pesa kwa ajili ya matibabu na kuagiza Halmashauri kusimamia suala hiyo.
‘’Kuanzia leo sitaki kusikia wala kuona wananchi wanalipa hiyo pesa ili watibiwe, haiwezekani mnawahamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya Afya halafu muwatoze fedha, hiyo pesa ambayo walikuwa wanaitoa kwaajili ya mlinzi, Halmashauri iwajibike’’ Amesema Shigela.
Katika hatua nyingine, Shigela ametoa ufafanuzi juu ya ujenzi wa barabara ya Malinyi - Ifakara ambapo amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania iko mbioni kutengeneza barabara hizo ili kuwarahisishia maendeleo wananchi wa Wilaya hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.