Wananchi wa Matuli Wilayani Morogoro waondokana na changamoto ya mawasiliano
Wananchi wa Kata ya Matuli Wilayani Morogoro Mkoani humo wameondokana na changamoto ya kukosa mawasiliano ya simu baada ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa fedha shilingi Milioni 125 kwa ajili ya kujenga mnara wa simu wa Kampuni ya Aiterl.
Hayo yamebainika Novemba 30 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Mnara huo uliojengwa katika Kijiji cha Matuli Kata ya Matuli Wilayani Morogoro, na kuzinduliwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji (MB)huku wananchi wakisimulia namna walivyokuwa wakipata changamoto katika kupata mawasiliano hayo ya simu.
Wamesema, awali wananchi hao walikuwa wanatumia makopo yaliyotundikwa kwenye mti ili kupata mtandao na kila aliyehitaji kupata mawasiliano ya simu alilazimika kutumbukiza simu yake kwenye moja ya kopo lililotundikwa juu ya mti na kuongea simu yake ikiwa imemening’inizwa kwenye mti huo.
Siku ya leo wananchi hao wameonesha furaha yao mara baada ya kuzinduliwa kwa mnara huo wa simu na kuanza kupata mtandao huku wakiongea na ndugu, jamaa na marafiki zao pasipo kutumia makopo bali wakiongea huku wakitembea barabarani, hivyo wameipongeza Serikali ya awamu ya sita na Mbunge wao Mhe. Hamis Taletale Maarufu kama Babu Tale kwa kupambana na kuwaondolea kero hiyo.
“Mbunge wetu katufanyia mambo hayo mazuri tunashukuru sana, tunampa pongezi na Serikali yetu kwa ujumla tunashukuru sana” alisema mwananchi mmoja wa Matuli aliyejulikana kwa jina la Omary Kamete.
Akiongea na wananchi wa Kijiji cha Matuli na vijiji jirani, wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi wa Mnara, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji ameeleza kazi ya Wizara yake kuwa ni kuhakikisha wanawafikishia wananchi huduma ya mawasiliano kwa asilimia kubwa na kwa uhakika ndani ya miaka mitano ya Serikali iliyoko madarakani.
“Na tunakwenda kuhakikisha ibara hizi mbili nilizozitaja tunazitekeleza kwa nguvu zetu zote….ibara hizi mbili zinatutaka tufanye yafuatayo; moja watanzania tuwafikishie huduma za mawasiliano kwa asilimia mia moja ndani ya miaka mitano hii…” amesema Dkt. Ashatu Kijaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema, pamoja na kutambua Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha nyingi za maendeleo Mkoani humo ikiwa ni pamoja na fedha za Barabara, Vituo vya Afya, Umeme na Fedha za Ujenzi wa Vyumba vya madarasa bado amesema kuwa ujenzi wa mnara huo, utaleta chachu kwa Familia na jamii nzima kwa ujumla hasa kiuchumi.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote hapa nchini (UCSAF) amesema jukumu la kupeleka mawasiliano kwa wananchi ni jukumu lao na hadi sasa wamekwisha peleka huduma hiyo katika kata laki moja na elfu sitini na nane kwa nchi nzima huku akiahidi kuwa UCSAF imejizatiti kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya Internet kutoka 45% hadi kufikia 80%.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya simu za Mkononi – Aitel, Jackson Mmbando amesema pamoja na changamoto ya ugumu kupata mawasiliano waliokuwa nao wananchi wa Matuli, wananchi hao walikuwa kwenye hatari kubwa hususan kwa upande wa usalama wa fedha zao.
Amesema wakala aliyekuwa anafanya kazi ya kutoa ama kuweka fedha ndani ya kijiji hicho alikuwa mmoja, na watu wote walijua kuwa wenye shida ya kutoa au kuweka fedha ni lazima wamtumie wakala huyo pekee jambo ambalo halikuwa jema kwa usalama wa fedha zao, hata hivyo amesema kampunia ya Airtel imemaliza changamoto hiyo na wako salama na huru sasa kutumia mtandao huo wa Airtel.
Imeelezwa kuwa jumla ya shilingi za kitanzania milioni 350 zimetumika katika ujenzi wa mnara huo hadi kukamilika kwake.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.