Wananchi wa eneo la Misegese katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro wameiomba Serikali kuwajengea Miundombinu ya barabara iliyopo katika eneo hilo ili kuwaondolea adha ya kusambaa kwa maji ya mto Fulwa uliovunja kingo zake na kumwaga maji yake katika eneo hilo.
Ombi hilo limetolewa na wananchi hao Januari 8 mwaka huu mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku nne ya kukagua utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarsa katika Shule za Sekondari ambapo wananchi wamepata nafasi kumweleza changamoto hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao akiwemo Joseph Amos, amesema barabara ya eneo hilo haipitiki kutokana na Mto Fulwa kuvunja kingo zake na kupelekea kuharibu miundombinu ya barabara hiyo na kusababisha adha kwa wananchi.
Naye, Hamza Mnunga, mkazi wa Malinyi ameiomba Serikali iwasaidie kurudisha miundombinu hiyo mapema kwa sababu barabara hiyo ndiyo barabara kuu inayotumiwa na wanafunzi kwenda shuleni na kuwapeleka wagonjwa katika hospitali ya Lugala.
‘’Hii ndiyo njia pekee ambayo tunaitegemea, tunayo shule na hospitali Lugala ambapo hii njia hutumika kutufikisha huko, kwa hiyo naiomba Serikali iweze kututatulia changamoto hii haraka’’ amesema Mnunga.
Kutokana na ombi hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akalazimika kufika katika eneo tukio na kushuhudia Mto huo namna ulivyoharibu miundombinu ya barabara ya eneo hilo
Aidha, Sanare amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo kuratibu kikao cha pamoja na baina ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Barabara Tanzania (TANROADS) ili kutafuta majawabu ya pamoja ya kutatua changamoto hiyo.
Katika hatua nyingine, Sanare amepiga marufuku magari kupita eneo ya daraja ambalo kwa sasa linajengwa kwa muda kutumia magogo makubwa na waendelee kudhibiti mpaka hapo watakapojiridhisha kukamilika kwa ujenzi huo.
’’Mvua sasa zimeanza kushika kasi sijui kama tutaweza kuwahi maana ilitakiwa tufanye mapema sasa hatukufanya…tuendelee kuhakikisha magari hayapiti hapa ni wananchi tu wanavuka mpaka hapo tutakaporekebisha na kujiridhisha tunaweza pitisha magari’’ amesema Sanare.
Kwa upande wake Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema katika kushughulikia changamoto hiyo ni muhimu kuanzia kwenye mto eneo ambapo maji yameanzia kusambaa na kama watabaini kuna uharibifu wowote unaofanyika basi hatua stahiki zichukuliwe.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Massele amesema hadi sasa wameshaandaa vifaa vyote kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambalo litajengwa kwa muda ili kurudisha mawasiliano kwa muda huku wakisubiria ujenzi wa daraja la kudumu.
Mwakilishi wa Mratibu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini -TARURA Mkoa wa Morogoro Luis Leopold amesema zaidi ya Shilingi Mil.55 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara hiyo kutengeneza mikondo itakayoongoza maji yapite kwenye madaraja watakayojengwa.
Hata hivyo, Luis amesema kwa sasa watashirikiana na uongozi wa Halmashauri hiyo ya Malinyi kutengeneza kivuko cha waenda kwa Miguu kisha daraja la kudumu litatengenezwa kuanzia Julai mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.