Wananchi wa Kijiji cha Namawala Wilayani Kilombelo Mkoani Morogoro wamemuomba Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela kutatua mgogoro wa shamba baina yao na mwekezaji mzawa anayejulikana kwa jina la Said Kambenga ambapo kila upande unadai kuwa shamba hilo ni mali yake.
Wananchi hao wametoa ombi hilo hivi karibuni walipokutana na Mkuu wa Mkoa huyo na kumueleza mgogoro huo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka mitano bila kupatiwa ufumbuzi huku wananchi hao wakilalamikia kupigwa, kushtakiwa mahakamani, kutishiwa maisha na mwekezaji kila wanapojihusisha na kilimo ndani ya shamba hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao akiwemo Bi. Shamila Ramadhani amesema kila msimu wa kilimo wanapoenda kulima katika eneo hilo ambalo walipewa na kijiji, Kambenga amekuwa akiagiza polisi kuwazuia wasiingie shambani au kuwapeleka rumande ama kuwafikisha mahamani na kuwafungulia kesi ya jinai kwa kosa la kulima katika shamba lake.
‘’…Hana vithibitisho vya kuonesha uhalali wa kumiliki hekari 1000 kama mwekezaji, akiambiwa aoneshe hati ya umiliki wa hekari 1000 hana, ana hati ya umiliki wa hekari 100 sasa tunashangaa inakuwaje anadai hekari 1000’’… alihoji Bi. Shamila.
Wakielezea chanzo chake, wananchi hao akiwemo Melisa Gozibert, amesema mgogoro huo umeanza mwaka 1996 ambapo mwaka 2020 waliwasilisha kero hiyo kwa aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara Mkoani Morogoro ambapo alimuagiza Mkuu wa Mkoa kuitisha kikao cha kutatua mgogoro huo.
Pamoja na Mkuu wa Mkoa kutekeleza agizo la kukutanisha pande hizo mbili ili kupata suluhu, bado hakukuwa na mwafaka kwa kuwa uchunguzi wa kupata nyaraka za umiliki wa shamba hilo ulihitajika zaidi ili kujiridhisha zaidi kuhusu mmiliki halali.
Kwa sababu hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Sanare kwa wakati huo alitoa maelekezo kwa Kambenga kutowasumbua Wananchi wenye mazao yao ndani ya shamba hilo hadi watakapovuna huku akimtaka naye kusitisha kuendelea kulima.
Aidha, Melisa amebainisha kuwa kijiji cha Namawala hakina mamlaka ya kumpa mwekezaji hekari 1000 na hakuwahi kulipia kodi ya shamba hilo tangu mwaka 2009 hadi sasa.
Kwa upande wake anayedaiwa ndiye mmiliki shamba hilo lenhye hekari 1000 Said Kambenga, amesema ana hati zote za kumiliki shamba hilo ambalo mahakama ya Ardhi ya Mkoa huo ilimpa umiliki wake tangu mwaka 2010 akiwepo Mwenyekiti wa Kijiji hicho ambaye kwa sasa ni marehemu.
Katika hatua nyingine, Kambenga amesema kutokana na wananchi kumuingilia katika shamba hilo na kuharibu mazao yake aliamua kuajiri kampuni ya ulinzi imsaidie kulinda shamba na kutoharibu mazao yake.
Akihitimisha mvutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewataka pande zinazohusika kuwa watulivu ili aunde timu itakayohusisha Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wataalamu wa Ardhi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na Uongozi wa kijiji, kwa lengo la kubaini maeneo yaliyolimwa ndani ya shamba hilo pamoja na wamiliki wake.
‘’…Tutabainisha maeneo yenye mgogoro ili tuje tuyatafutie ufumbuzi, kwenye maeneo ambayo hayana migogoro, yale yenye migogoro tuyatafutie ufumbuzi na yale ambayo hayana tuyaache kwenye mlolongo mwingine…’’ amesema Shigela.
Sambamba na maagizo hayo, Shigela ameagiza kusiwepo na mtu yeyote wa kufanya shughuli zozote za kilimo katika shamba hilo mpaka pale kamati yake itakapofanya utafiti na kujiridhisha na kuwaletea majibu ya kamati yake na kuhitimisha mgogoro huo rasmi.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.