Wakazi wa Morogoro waunga mkono wavamizi vyanzo vya maji kuondolewa
Wakazi wa Mkoa wa Morogoro wamekubali na kuunga mkono zoezi la kuwaondoa watu waliovamia vyanzo vya maji vilivyoko katika milima ya Ulugulu zoezi litakaloanza muda wowote, lengo likiwa ni kutunza vyanzo hivyo ili kuondoa changamoto ya uhaba wa maji katika maeneo mengi ya Mkoa huo.
wakazi wa Kata ya kihonda
Wananchi hao wametoa kauli hiyo Septemba 13, 2022 walipoulizwa swali hilo na Mkuu wa Mkoa huo Fatma Abourbakar Mwassa wakati wa Mkutano wa hadhara Kata ya kihonda Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kujitambulisha rasmi, kutembelea miradi ya maendeleo na kutatua kero za wananchi ndani ya Mkoa huo.
“sasa tufike mahali tukubaliane, tuache hawa wanaochaguliwa wasihujumiwe au tuwaondoe kule ili tupate maji? Ndugu wananchi mnasemaje,” Fatma Mwassa alihoji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa wakati wa Mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Kihonda
Mkuu huyo wa Mkoa amesema tatizo kubwa la uhaba wa Maji katika Manispaa ya Morogoro sio miundombinu bali ni wananchi wenyewe wa Morogoro ambao baadhi yao wameamua kuharibu kwa makusudi vyanzo vya maji, kwa kufanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo hivyo na kukausha vyanzo au kuchepusha maji kwenye mito na kusababisha maji kutofika kwenye miundombinu hivyo wananchi kukosa maji.
Aidha, Fatma Mwassa amesema inapofika wakati Serikali inataka kuchukua hatua dhidi ya uvamizi hiuo baadhi ya wana siasa huingiza siasa kuwa wanahujumiwa hali iliyopelekea Kiongozi huyo kuamua kushirikisha wananchi na kutoa maoni yao, lipi jema, kuwandoa wavamizi wa vyanzo vya maji ili wananchi walio wengi wapate maji au kuwatetea wapiga kura wachache wa wanasiasa na kukosa maji swali ambalo wananchi wamechagua wavamizi waondolewe kwenye vyanzo vya maji.
Amesema, ili kuondoa changamoto hiyo ya maji katika Mkoa huo hususan Manispaa ya Morogoro ni suala la kukubaliana na kuamua kwa pamoja Kuhifadhi vyanzo vya maji, kuviheshimu na kuvilinda kwa nguvu zote kwani amesema, kadri suala hilo linapozidi kufumbiwa macho ndivyo changamoto ya maji inazidi kuwa mbaya zaidi.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan tayari imetoa fedha kiasi cha shilingi 12Bil. kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro peke yake, miradi hiyo ni ile itakayotekelezwa kwa muda mfupi na muda mrefu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuongea na wananchi wa Kata ya Kihonda
Diwani wa Kata ya Kihonda, Mhe. Hamis Kilongo pamoja na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kupeleka fedha nyingi katika Kata hiyo kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Afya, Elimu na Maji bado amemuomba Mkuu wa Mkoa huo kuwasaidia wananchi wa Mtaa wa Azimio wanaokabiliwa na kero ya kujaa maji ya mvua katika eneo lao huku Mtaa wa Kiegea wakikabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara na kwamba maeneo yote mawili yanahitaji Greda kwa ajili ya kurekebisha maeneo hayo.
Diwani wa Kata ya Kihonda
Taarifa ya hali ya maji katika Manispaa ya Morogoro iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira manispaa ya Morogoro (MORUWASA) imeeleza kuwa Ofisi hiyo kwa kushirikiana na Wadau wengine wa maji wamebaini hazina ya maji chini ya Ardhi eneo la Dakawa yanayoweza kutosheleza matumizi ya maji kwa watu wote wa Mkoa wa Morogoro hadi mwaka 2040.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando akimkaribisha Katibu Tawala wa Mkoa kusema machache na kisha amkaribishe Mkuu wa Mkoa
Taarifa ya hali ya maji katika Manispaa ya Morogoro iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira manispaa ya Morogoro (MORUWASA) imeeleza kuwa Ofisi hiyo kwa kushirikiana na Wadau wengine wa maji wamebaini hazina ya maji chini ya Ardhi eneo la Dakawa yanayoweza kutosheleza matumizi ya maji kwa watu wote wa Mkoa wa Morogoro hadi mwaka 2040.
Kwa upande wao wananchi wa Kata ya Kihonda, akiwemo Bibi Asha Malekela kutoka Kiegea “A” amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro changamoto kubwa ya uhaba wa maji wanayoipata huku akimuomba Kiongozi huyo kusaidia kutatua changamoto hiyo inayowakabili wakazi hao.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.