Wananchi wa Kata ya Boma katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wameunga Mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuunganisha nguvu zao na Halmashauri kujenga Shule mpya ya Sekondari inayotarajiwa kukamilika kabla ya tarehe 28 Februari mwaka huu kwa kujenga vyumba 10 vya madarasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti hivi karibuni wananchi wa Kata ya Boma, wamesema wamesumbuka kwa muda mrefu kutafuta sehemu ya karibu kwa ajili ya ujenzi wa Shule hiyo, hivyo wameishukuru serikali kwa kuwapatia eneo ambalo lipo katika kata yao na kuahidi kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa shule hiyo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Boma Athuman Omary, amesema ameunga mkono jitihada za Serikali kutokana na imani kubwa aliyo nayo juu ya Serikali ya awamu ya tano, laikini pia kwa lengo la kuwezesha miundombinu rafiki kwa wanafunzi ili wasitembee umbali mrefu kufika Shuleni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Afisa Elimu wa Halmashauri hiyo Dkt. Janeth Balongo amesema Shilingi Mil.578 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo huku shilingi Mil. 100 zikiwa tayari zimewekwa katika akauti yao kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
Aidha, Dkt. Balongo amesema shule hiyo itakuwa ni shule shikizi kwa sasa na kwamba itachaguliwa shule moja ambayo itailea kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa mwaka huu na baada ya kukamilisha ujenzi itakuwa shule maalumu kwa ajili ya masomo ya Sayansi.
Akizungumza na wananchi wa Kata hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo aliyefika eneo la ujenzi kwa lengo la kukagua na kuhamasisha ujenzi huo, ameipongeza Halmashauri hiyo kwa uamuzi wa kujenga shule mpya na kwa ubunifu wao wa kuamua kujenga madarasa hayo kwa mtindo wa ghorofa.
“... Na leo nimesikia Manispaa wanaanzisha ujenzi wa shule mpya ambayo kabla ya Februari 28 mwaka huu itakuwa na vyumba kumi vya kutosha, nawapongeza sana Manispaa…..lakini bado wanasema kwa sababu sisi tupo Mjini hatuwezi kujenga ujenzi wa kawaida, watajenga majengo ya ghorofa tatu tatu hapa… alisema Mhandisi Kalobelo.
Aidha, Mhandisi Kalobelo amesema shule hiyo itakuwa ni ya mfano ambayo itahusika na masomo ya Sayansi lakini pia wanafunzi watapata nafasi ya kusoma Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wakiwa shuleni hapo.
Morogoro ni miongoni mwa Mikoa ambayo imefanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa darasa la saba ambapo mwaka huu 2020 imeshika nafasi ya nane Kitaifa kutoka nafasi ya 16 mwaka 2019. Mkoa unaendelea kujipanga kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu darasa la saba 2020 wanajiunga na kidato cha kwanza mapema mwaka huu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.