Waananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Mkoani Morogoro wameafiki agizo la Serikali la kuhama katika eneo la hifadhi katika Bonde la Mto kilombero Ili kumuunga mkono Dkt. John Pombe Magufuli katika azma yake ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Mwalimu nyerere ambao asilimia 62 ya Maji yatakayoendesha mradi huo yanatokana na hifadhi hiyo.
Hayo yamebainishwa Disemba 16 Mwaka huu na baadhi ya Wananchi wa Wilaya hiyo, walipohojiwa na vyombo vya habari baada ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mathayo Maselle kueleza azma ya Serikali ya Wilaya hiyo kukusudia kuwaondoa wavamizi wote wa bonde hilo la hifadhi alipokuwa akifungua kikao cha kwanza cha wahe. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi.
Wananchi hao akiwemo Bi. Maija Amrani wa Kijiji cha Ngohelanga wamesema hawaungi mkono wananchi wenzao kuendelea kufanya shughuli za kibinamu ndani ya eneo la hifadhi kwa kuwa wanaharibu vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na mradi mkubwa wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere ulioazishwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao unaenda kuleta unafuu kwa wananchi katika kupata nishati ya hiyo ya umeme.
“….lakini ilishasemwa kwamba wanaokaa karibu na vyanzo watoke, na hasa wale wanaokaa kuanzia chini ya mwaka 2017 kurudi chini wale wote wa nyuma watoke, lakini lile la mwaka 2012 kuja huku lina ruhusa watu waendelee kulitumia, kwa hiyo ni vyema kutoka katika hifadhi ili kuunga mkono jitihada za Rais wetu….” Amesema Amrani
Naye January Silvester amesema eneo hilo limekuwa likivamiwa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali huku baadhi yao wakijimilikisha maeneo makubwa katika hifadhi hiyo kinyume na sheria, hivyo wanaunga mkono agizo la serikali la wavamizi hao kuondoka katika hifadhi ya Bonde la Mto Kilombero licha ya changamoto watakazokumbana nazo katika kuhamia maeneo mapya.
Akizungumza katika Kikao cha baraza hilo Mkuu wa Wilaya hiyo Mathayo Masele aliyekuwa Mgeni rasmi amesema eneo la hilo la hifadhi linachangia kwa asilimia 62 ya maji yote yanayoelekea katika bwawa la Mwalimu Nyerere, hivyo wananchi wanaoishi katika hifadhi hiyo hawana budi kuhama ili kupisha ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya alitaja mikakati iliyopo ya kuhakikisha watu waliovamia maeneo ya hifadhi wanaondoka kwa amani ni pamoja na kutoa Elimu juu ya umuhimu wa Bonde hilo la Mto Kilombero.
Mikakati mingine ametaja kuwa ni kutoa Elimu juu ya kubadili mtindo wa kilimo, kulima eneo dogo lakini linaloweza kutoa mavuno ya kutosha, kubadili aina ya mazao ya kulima badala ya kuamini kilimo cha mpunga pekee. Mkakati mwingine ni wananchi kujikita katika kilimo cha umwagiliaji kwa kutumia Skimu za umwagiliajo zilizopo na kuanzisha nyingine mpya.
Maafisa kutoka Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro Crister Njovu (kulia) na Marcelin Ndimbwa wakijadili jambo wakati wa Kikao hicho
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Pius Gerlad amesema Serikali iangalie uwezekano wa kutoa eneo la kipande cha hifadhi linalopatikana kati ya mipaka ya mwaka 2012 na 2017 ili liwasaidie wananchi watakao hamishwa kutoka maeneo ya hifadhi hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.