Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe, Adam Kighoma Malima amewataka wafanyabiashara na Wajasiriamali wanaodaiwa malimbikizo ya kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA kutakiwa kuyalipa madeni hayo ili kukuza uchumi wa Taifa na hivyo Taifa kujitegemea.
Adam Malima ametoa gizo hilo septemba 22 mwaka huu wakati akifungua Kampeni ya TUWAJIBIKE ngazi ya Mkoa iliyoandaliwa na TRA na kufanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa Mkoa huo huku kikiwashirikisha Baraza la Wafanyabiashara na wajasiliamali TCCIA.
Akitoa agizo hilo wakati akifungua kampeni hiyo iliyolenga kuhimiza wafanyabiashara kutoa risiti kwa kutumia mashine ya kielektroniki na wananchi kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa zao, amesema wafanyabiashara wanapochelewa kulipa madeni hayo wanazidi kuongeza riba na madeni kuzidi kuongezeka zaidi kisha kupeleka lawama kwa TRA.
“Lakini mjihisi na mjichukulie kwamba na nyinyi mnawajibu wa kulipa malimbikizo hayo, mnapochelewa kulipa malimbikizo hayo mnaongeza riba na mwisho wa siku madeni haya yanazidi kuongezeka” amesema Mhe, Malima.
Hata hivyo, ameipongeza TRA kwa kutambua mchango wao katika kukusanya mapato jambo ambalo linainua uchumi wa wananchi na nchi kuweza kujitegemea kiuchumi.
Kwa upande wake Kaimu meneja TRA Mkoa wa Morogoro Bw. Chacha Gotora amesema wamezindua kampeni ya tuwajibike kwa lengo la kuhamasisha wafanyabiashara kutumia mashine za kielectroniki na wateja kudai risiti sahihi wanapo nunua bidhaa ili kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa maslahi ya Taifa.
Nao wananchi wa Mkoa wa Morogoro akiwemo Bw. Joshua Mkazi wa Manispaa ya hiyo ameishukuru TRA kwa kampeni hiyo ya TUWAJIBIKE huku akieleza kuwa TRA inatoa elimu nzuri kwa wateja wake juu ya umuhimu wa kutoa kodi na kudai risiti ya kielektroniki kwa maendeleo ya taifa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.