Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema miongoni mwa makundi yanayochangia ukuaji wa Uchumi wa Mkoa huo ni kundi la wanawake, hii ni kutokana na kundi hilo kuwa na ushiriki mkubwa katika shughuli za kimaendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mhe. Malima amesema hayo Machi 8, 2024 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambapo kimkoa maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya shule ya Msingi K/ Ndege iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amewapongeza Wanawake wa Mkoa huo kwa jitihada za kuendeleza maendeleo ya Mkoa huo na kubainisha kuwa Mkoa unasongambele kwa kasi pia amesema Mkoa una malengo mbalimbali ya kimaendeleo ambapo wananwake hao ndiyo msingi wa kuyafikia malengo hayo.
“...niwapongeze akina mama wote wa Morogoro kwa kazi na jitihada mnazofanya katika kuleta maendeleo ya Mkoa wetu...akina mama ni msingi wa mafanikio ya Mkoa wetu wa Morogoro...” amesema Mhe. Adam Malima.
Aidha, Mhe. Malima amesema Taifa lisiloheshimu mchango na nafasi ya wanawake katika shughuli za maendeleo basi Taifa hilo litakuwa limedumaa huku akieleza kuwa uwekezaji kwa wanawake unaibadilisha jamii moja kwa moja.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa ametumia maadhimisho hayo kuwataka wananchi wa Mkoa huo kuachana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ulawiti huku akiweka bayana kuwa Mkoa umejipanga kwa dhati kukomesha vitendo hivyo.
Sambamba na hilo amezitaka taasisi zinazohusika na utoaji wa haki kuendelea kutoa elimu juu ya haki za wanawake hususan walio katika mifumo ya ukatili wa kijinsia.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro Bi. Susan Kihawa amesema Mahakama ya Tanzania imefanya maboresho mbalimbali kwenye sheria na haki za wanawake huku akisema kuwa ukombozi wa kifikra na Elimu madhubuti ni jambo linalotakiwa kutiliwa mkazo ili wanawake waweze kutambua haki zao.
Akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa huo Bi. Sophia Kalinga amesema uwekezaji kwa wanawake ni sawa na kuwekeza kwa jamii kwani mwanamke ni mlezi wa familia anayesimamia malezi na maadili kwa Watoto lakini pia anatunza uchumi wa familia, hivyo jamii inapaswa kuwa na mtazamo chanya kwa wanawake kuwa wanauwezo sawa na wanaume.
Aidha, Bi. Sophia ameishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga shule maalumu za wasichana kila Mkoa ambapo Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyonufaika hivyo wanawake watapata fursa ya elimu ambayo ndiyo mkombozi wa mwanamke.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.