Wanufaika wa TASAF kuwa na mwelekeo wa kujitegemea.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Mpango wa kunusuru Kaya Masikini Tanzania - TASAF Dkt. Charles Mwamwaja amesema kuwa mwelekeo wa TASAF kwa sasa ni kuona kuwa wanufaika wa mpango huo wanakua, wanaendelea na mwisho wanajitegemea kiuchumi.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Mpango wa kunusuru Kaya Masikini Tanzania - TASAF Dkt. Charles Mwamwaja na ujumbe wake akiongea na wananchi wa kijiji cha Mkambarani
Dkt. Mwamwaja amesema hayo Disemba 13 mwaka huu wakati wa ziara ya Wajumbe wa Bodi hiyo Moani humo ambapo Pamoja na shughuli nyingine wametembelea miradi inayotekelezwa na TASAF ukiwemo mradi wa zahanati iliyojengwa na TASAF awamu ya kwanza katika Kijiji cha Mkambarani.
baadhi ya wajumbe wa Bodi wakiwa katika kikao hicho
Akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mkambarani kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Dkt. Mwamwaja ameonesha kufurahishwa na uanzishwaji wa vikundi vya ujasiliamali ndani ya wanufaika wa Mpango huo na kwamba kupitia vikundi hivyo wanaweza kunufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri au hata ya kutoka Serikali Kuu hivyo kujinusuru na umaskini waliokuwa nao awali.
baadhi ya wanufaika wa kijiji cha Mkambarani
Kwa sababu hiyo Dkt. Mwamwaja amewahamasisha wanufaika hao kuendeleza vikundi hivyo ambavyo vingine vinatengeneza sabuni na kuwahakikishia kuwa huo ndio mwelekeo wa TASAF kutaka wanufaika kutumia kile kidogo wanachopata kukiendeleza na mwisho waweze kujitoa kwenye umasikini na kujitegemea.
“huo ndio mwelekeo, tungependa hawa wenzetu tuwaunge mkono, huko wanakoelekea wataanzisha vikundi…. vikikua vitafika mahala vitafanya ujasiliamali mdogomdogo…..vitanufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri na baadae inayotolewa na Serikali” amesema Dkt. Mwamwaja
Mwenyekiti akinunua sabuni zilizozarishwa na moja ya vikundi vilivyoanzishwa kujinusuru na umaskini
Pia amesisitiza kuwa furaha ya mzazi sio tu kumlea mtoto zaidi kuona mtoto anafika mahali anajitegemea, na hilo ndilo lengo la TASAF la kuwataka kuwanusuru wanufaika kwa kuwapa fedha kidogo na maarifa hatimaye waweze kujitegemea wenyewe.
“neno letu ni kwamba tutahakikisha tunamlea, anakua ili kesho na kesho kutwa furaha ya mzazi si kumwona mtoto anajitegemea! kwa hiyo tutamlea tutahakikisha anakua ili kesho na kesho kutwa na yeye aanze kujitegemea” amesisitiza Dkt. Mwamwaja
sabuni zinazotengenezwa na kikundi baada ya kupata mafunzo na utaalamu chini ya uratibu wa TASAF
Aidha, amewatoa hofu wanufaika hao kuwa, TASAF itaendelea kusaidia walengwa wanaokizi vigezo kwa lengo la kupiga vita umasikini na hatimaye kuona wanajikwamua na kisha kujitegemea kiuchumi.
Akiwa katika kikao cha Pamoja na uongozi wa Mkoa na Wilaya katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Mwamwaja amesema miradi inayoanzishwa na TASAF ni miradi ya Serikali hivyo inatakiwa kushughulikiwa kama miradi mingine ya Serikali kwa kuwa lengo la TASAF ni kuondoa adui umaskini miongoni mwa watanzania lengo ambalo linatekelezwa pia na Serikali Kuu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Martine Shigela Pamoja na kutoa shukrani kwa Wajumbe wa Bodi ya TASAF kutembelea Mkoa huo, amewataka Waratibu wa TASAF Wilaya na Mkoa Mkoani humo kuendelea kutoa Elimu muda wote juu ya vigezo vinavyomuingiza mnufaika kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando
Amesema kuacha wananchi peke yao kuchaguana kutaendeleza malalamiko kwa sababu wengeni wanaweza kuingizwa kwenye mpango kisiasa au kwa ushawishi hivyo kutotatua malalamiko ya suala la TASAF kama ambavyo hujitokeza karibu kila mikutano ya hadhara.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya masikini ngazi ya Mkoa, Mratibu wa TASAF Mkoa wa Morogoro Jacob Kayange ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa wanufaika wa mpango huo kupitia ruzuku wanayopata kuwa imewasaidia baadhi yao kupata maeneo ya kulima hivyo kuongeza kipato.
Mratibu TASAF Mkoa wa Morogoro Bw. Jacob Kayange akitoa maelezo juu ya utekelezaji wa TASAF Mkoani humo
Mafanikio mengine ni Pamoja na wanufaika kuanzisha biashara ndogo ndogo, kujiunga na CHF kwa lengo la kujiwekea akiba kwa ajili ya matibabu, kuhudumia mahitaji ya Watoto shuleni na mpango umewezesha kuongeza mahudhurio mazuri ya Watoto shuleni kutokana na kaya hizo kupata ruzuku ya fedha kutoka kwenye mpango huo.
Zahanati ya Mkambarani iliyojengwa na TASAF awamu ya kwanza
Ujenzi wa maabara na Wodi ya mama na mtoto katika zahanati ya Mkambarani ukiendelea
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya TASAF Taifa Dkt. Charles Mwamwaja akikagua ujenzi wa Miundombinu inayoendelea kujengwa katika zahanati ya Mkambarani
Wakitoa ushuhuda wao mbele ya Wajumbe wa Bodi ya TASAF, wanufaika wa mpango huo kutoka Kijiji cha Mkambarani wametoa shukrani zao kwa Bodi hiyo kwa kuwajengea zahanati ya Mkambarani ambayo kwa sasa imeingiziwa fedha tena zaidi ya shilingi Mil. 188 kwa ajili ya kujenga maabara na wodi ya mama na mtoto katika zahanati hiyo.
shuhuda wa Mpango wa kunusuru kaya masikini akishuhudia jinsi alivyofaidika na mpango huo
Aidha, wamekiri kuwa TASAF imewasaidia kwa kiwango kikubwa, kwanza kwa kuwapa fedha zilizowawezesha kuanzisha miradi kwa mtu mmoja mmoja na baadae kuazisha vikundi vya Pamoja vya ujasiliamali vya Faraja na Tushikamane ambavyo vinawasaidia katika kusomesha Watoto na kujipatia mahitaji muhimu.
Shuhuda
Ombi lao wananchi hao ni moja tu, TASAF iendelee kuwalea lakini pia kuwaingiza kwenye mpango huo wazee wengine waliopo katika Kijiji cha Mkambarani na maeneo mengine hasa wale wanaokidhi vigezo vya kuingia kwenye mpango ili kuondoa malalamiko ambayo yameendelea kuwepo ndani ya TASAF.
Mpango wa TASAF awamu ya kwanza katika Mkoa wa Morogoro umetekelezwa katika Halmashauri mbili za Morogoro na Ulanga, TASAF awamu ya pili ilihusisha halmashauri sita za Morogoro DC, Manispaa ya Morogoro, Kilosa, Kilombero, Ulanga na Mvomero na awamu ya tatu mpango ulianza rasmi mwaka 2012 na Morogoro umeanza mwaka 2013 na kwa awamu hiyo jumla ya shilingi Bi.10.23 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo kwa walengwa wapatao 47,124.
Baadhi ya viongozi wakimsikiliza Dkt. Mwamwaja akiongea na wanufaika wa Mkambarani. kushoto ni Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Morogoro Anza Amen Ndossa
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.